1. Ripoti: Uhasama wa umma dhidi ya wabunge waongezeka duniani 

Wabunge kote ulimwenguni wanakabiliwa na viwango vinavyoongezeka vya vitisho, unyanyasaji na vurugu kutoka kwa umma imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na Muungano wa Mabunge Duniani (IPU) yenye jina la Umma unapogeuka kuwa maadui: Vurugu za kisiasa dhidi ya wabunge

IPU ambayo inajumuisha mabunge 183 na vyombo 15 vya bunge vya kikanda imefanya utafiti kwa kina katika nchi 5 wanachama ambazo ni Argentina, Benin, Italia, Malaysia na Uholanzi ambapo jumla ya wabunge 519 walihojiwa lengo likiwa nikuonesha mwelekeo wa kimataifa katika mazingira tofauti ya kisiasa.

Ripoti hiyo yenye kurasa 80 imebainisha pamoja na mambo mengine kuwa: – 

  • Asilimia 71 ya wabunge walioshiriki wameripoti kukumbwa na aina fulani ya vurugu kutoka kwa umma, iwe mtandaoni, nje ya mtandao au vyote kwa pamoja. 
  • Vurugu nyingi zinatokea mtandaoni, ambapo kati ya asilimia 65 na 77 ya wabunge katika nchi hizo waliripoti kutukanwa, kudhalilishwa, kusambaziwa taarifa za uongo au kutishiwa. 
  • Wabunge wengi wanaamini hali inaendelea kuwa mbaya, huku wabunge 8 kati ya 10 nchini Argentina na Uholanzi wakisema vurugu zimeongezeka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
  • Ripoti inaeleza kuwa wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume. Asilimia 76 ya wabunge wanawake wameripoti kukumbwa na vurugu ikilinganishwa na asilimia 68 ya wanaume. 
  • Wabunge kutoka makundi yanayowakilisha walio wachache au yaliyo hatarini, wakiwemo wenye ulemavu na jamii za LGBTQIA+, wako kwenye hatari kubwa zaidi.
Lakini sababu kubwa ya wananchi kujenga chuki ni nini hasa?

Ripoti hiyo ya IPU inaeleza kuwa kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa, mashinikizo ya kiuchumi na kijamii, pamoja na kupungua kwa imani kwa taasisi za umma, vinachochea uhasama huo.

Ripoti imeonya kuwa vitisho vinaweza kudhoofisha demokrasia kwa kuwafanya wabunge kujinyima uhuru wa kujieleza, kuepuka mikutano ya umma au hata kuacha kugombea. 

Nini kifanyike?

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo 18 ya nini kifanyike ikiwemo kuzidisha uwazi, kufanya kampeni za kujenga uelewa na mbinu mbalimbali za kujilinda mitandaoni na nje ya mitandao ya kijamii. 

IPU inatoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuweka mipaka ya mazungumzo ya umma na kulinda sauti za wachache.

Hitimisho la ripoti hiyo ni kuwa vurugu za kisiasa zinazofanywa na umma dhidi ya wabunge ni jambo la kimataifa linaloenea katika maeneo, tamaduni na mifumo ya kisiasa kila mahali, mwelekeo unaonesha dhahiri, hakuna bunge linaloweza kusema wao wanakinga. Na hii inafanya vurugu za kisiasa kuwa si suala la ndani ya nchi bali ni changamoto ya kimataifa, ambayo inafanya ushiriki wa pamoja wa uzoefu ili kulinda taasisi za kidemokrasia na wawakilishi wanaoziunga mkono kuwa jambo muhimu.

Mwanamke mwenye tabasamu kutoka Tanzania akiwa amevaa kanzu nyeupe ya daktari mwenye lebo ya jina, amesimama ndani ya nyumba katika mazingira ya kitaalamu.

Dkt. Mugara ni Mkunga mbobevu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, ambaye pia ni mwanasayansi mwanamke.

2. Wanawake sayansi tunaiweza kinachotakiwa ni kujiamini: Dkt. Mugara Mahungururo

Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi mwaka huu mauadhui yakihimiza “Sayansi kwa Mustakabali Jumuishi kwa Wanawake na Wasichana” Kwamujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , Sayansi na Utamaduni UNESCO leo hii , wanawake wanachangia chini ya theluthi moja ya watafiti duniani, kulingana hivyo kuziba pengo hili la kijinsia si suala la haki pekee ni muhimu kwa ubora, uhalisia na mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu. 

Dkt. Mugara  Mahungururo ni Mkunga  mbobevu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Ni miongoni mwa asilimia 35 pekee ya wanawake wahitimu wa sayansi duniani kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataofa la Elimu Sayansi na Utamadini UNESCO. Nini limvutia hadi kuingia kwenye tasnia hii ya sayansi inayotawaliwa na wanaume ?

“Mimi ni mwanasayansi kikubwa kilichonivutia kujiunga katika sayansi ni kutokana na mazingira ambayo nimekulia. Niliishi mazingira ya hospitali. Nilishuhudia wazazi wangu na ndugu na jamaa wakitoa huduma kubwa kwa watu waliokuwa wanakuja kwa uhitaji mbalimbali hapa hospitalini. Nikajiunga na masomo ya sayansi nikiwa sekondari . Baada ya hapo nikajiunga na chuo.”

Baada ya kuhitimu na kuwa mkunga mmbobezi kazi inayompa faraja na kujivunia sana 

Dkt. Mugara anasema kama yeye ameweza basi wanawake na  wasicha wengine nao wataweza pia 

“Kwa upande wa masomo ya sayansi. Natamani sana wasichana na wanawake wengine wajue kabisa kwamba wakitia nia hakuna kitu kigumu. Ukitia nia na ukikazana jitihada zako zote zitakuja kuleta matunda chanya. Kwa hiyo niwatie moyo wale wote wanaotaka kusoma sayansi ikiwa wana lengo la kukamilisha kitu fulani katika maisha yao. Kuipa jamii kusaidia katika nyanja tofautitofauti kuleta matokeo chanya. Waende kusoma sayansi sio ngumu. Tia nia na jitihada. Pambana utafanikiwa kufikia malengo yako unayotamani.”

Anamalizia kwa wito , siku zote samaki mkunje angali mbibichi kwani akishakauka hakunjiki

“Nadhani katika sayansi ili tuweze kuongeza idadi ya wanawake tusianze ngazi za juu, tuanzie kuwapa moyo wanafunzi kuanzia shule za msingi wajue sayansi ni nini wajue wakisoma masomo gani yatapelekea wao kuwa kina nani watambue kwamba wanataka kuwa akina nani? Kuna watu watachagua kuja kufanya masomo ya sayansi, tukuze ndoto zao kwa kuwapa msaada na ufahamu mitaala ipo. Mitaala iliyopo sasa hivi inasapoti watoto wetu kujifunza vizuri wazazi pia nyumbani. Tusikilize ndoto za watoto wetu wanaotaka kuja kwenye sayansi. Tuwasaidie. Wasichana msikate tamaa inawezekana. Inawezekana kuwa mwanasayansi inawezekana kuwa mwanasayansi mkubwa sana katika hii dunia, lakini tuanze pia katika jamii yetu hatua moja inatengeneza nyingine.”

Mwanamume katika suti na tai akizungumza katika hafla iliyo na mandhari ya 'Kuongeza kasi ya kupitishwa kwa watoto' na alama ya UNDP.

Mjumbe Maalum wa Masuala ya Teknolojia kwenye Ofisi ya Rais wa Kenya Balozi Philip Thigo akizungumza na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa jijini Nairobi kuhusu AI.

3. Fungueni minyororo ya kihistoria inayokwamisha Afrika

Jukwaa la akili unde au AI lililofanyika kwa siku mbili huko Nairobi, nchini Kenya limekunja jamvi ambapo mmoja wa washiriki amesema wanaodai kuwa bara la Afrika liko nyuma kwenye teknolojia hiyo, ni dhahiri shairi hawalifahamu vema bara hilo lenye mataifa 54. 

Mjumbe Maalum wa Masuala ya Teknolojia kwenye Ofisi ya Rais wa Kenya Balozi Philip Thigo akizungumza na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, amesema..

“Afrika hakika iko kwenye mustakabali wake,  na akili unde  au AI ni teknolojia halisi kwa bara la Afrika kwa sababu AI ni shirikishi na inabadilika haraka kwa sababu ya kasi yake. Na bara hili kama tunavyofahamu linakua kwa kasi kubwa na ni bara changa. Na pia bara hili ni mustakabali wa dunia iwapo utaangalia demografia yake. Kwa hiyo pale kila mtu anaposema Afrika iko nyuma, sisi tunasema hawalielewi hili bara. Kwa sababu kitu ambacho bara hili linahitaji ni kufunguliwa minyororo ya kihistoria ambayo imekuwa ikiliengua na fursa . Kile tunahitaji ni fursa.”

Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na serikali ya za Italia na Kenya pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP.

Mwanamke akizungumza katika Jukwaa la Nairobi AI Forum, akiwa na bendera ya kijani inayoonyesha jina la tukio na nembo nyuma.

Giulia Vitagliano, Meneja wa Mikakati na Ushiriki wa kitengo cha UNDP kinachohusika na AI kwa Maendeleo Endelevu, AI Hub for Sustainable Development.

Meneja wa Mikakati na Ushiriki wa kitengo cha UNDP kinachohusika na AI kwa Maendeleo Endelevu, AI Hub for Sustainable Development, Giulia Vitagliano akitoa tathmini ya mkutano huo amesema kulikuweko na washiriki zaidi ya 500.

Akielezea kitengo chake amesema;

“Tunashirikiana na vijana  wenye miradi ya kuanzisha biashara pamoja na mitaji ya uwekezaji ili kuleta mabadiliko ya kweli—kuimarisha misingi ya akili unde, data, kompyuta, na vipaji. Tunatazamia kupokea maombi na michango yenu ya ushiriki, na tunatoa fursa nyingi za kipekee. Tafadhali tembeleeni tovuti ya Vituo vya AI kwa Maendeleo Endelevu, na pia angalieni shughuli za UNDP kupitia mitandao yetu ya kijamii na tovuti zetu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *