Zaidi ya huduma za kibingwa 3,000 zatolewa siku 100 za Rais SamiaZaidi ya huduma za kibingwa 3,000 zatolewa siku 100 za Rais Samia

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (Upanga na Mloganzila) imefanikiwa kuwasogezea wananchi zaidi ya 3,000 huduma za kibingwa katika kipindi cha siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, jambo linaloashiria utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuwanufaisha wananchi kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk. Delilah Kimambo ameeleza jinsi kampasi zote mbili za hospitali zinavyoshirikiana na wadau wa maendeleo kupanua wigo wa huduma na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma.

“Katika kipindi hiki, hospitali imetekeleza huduma za kibingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa uroto, figo, nyonga na magoti, huku tukiendelea na maandalizi ya mwisho ya kuanza upandikizaji wa ini,” amesema Dkt. Kimambo. SOMA: Muhimbili yaboresha ubebaji wagonjwa wasioweza kujihudumia

Aidha, Dk. Kimambo ameongeza kuwa hospitali inatekeleza kwa ufanisi agizo la kutozuia miili hospitalini kutokana na madeni na sasa kuna utaratibu maalum unaoruhusu familia kuchukua mwili wa mpendwa wao hata kama gharama za matibabu hazijakamilishwa.

Pia amewataka wananchi kuchangamkia bima ya afya kwa wote ambayo itarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati, kuondoa usumbufu wa madeni na kuhakikisha familia hupata huduma bila kikwazo pale wapendwa wanapopoteza maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *