
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imeingia makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu na Kituo cha Kukuza Uadilifu na Uwajibikaji wa Masuala ya Fedha (CIFA–Tanzania) kwa lengo la kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika mashirika ya umma.
Akizungumza leo Februari 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waheed Muhammad Ibrahim amesema mkataba huo unaweza kuongezwa baada ya kumalizika kwa muda wake.
Amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar ilianzishwa mwaka 2022 kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya mwaka 2021, inayomtaka msajili kusimamia na kuimarisha utawala bora katika taasisi za umma.
“Utawala bora hauwezi kuwepo bila utendaji mzuri. Ofisi yetu imeona umuhimu wa kushirikiana na CIFA kusimamia na kuimarisha misingi ya utawala bora katika taasisi zetu. Huu ni msingi muhimu kwa maendeleo ya mashirika ya umma,” amesema.
Ameeleza kuwa mkataba huo utaziwezesha bodi za taasisi za umma kufahamu vyema wajibu wao na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji.
“Bila taasisi kufahamu na kuzingatia misingi ya utawala bora, suala la uadilifu litakuwa changamoto,” amesema.
Msajili huyo amesema ofisi yake tayari imeanza kuweka viashiria vya kupima utendaji wa taasisi kupitia bodi zao, huku bodi zikitakiwa kuweka viashiria hivyo kwa wakurugenzi wa taasisi husika.
Ameongeza kuwa mbali na kusimamia utawala bora, makubaliano hayo yatahusisha utoaji wa mafunzo yatakayolenga kuinua utendaji na kusaidia taasisi kufikia malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salehe Hamad Saleh amesema utawala bora ni nguzo muhimu ya maendeleo ya mashirika ya umma.
“Utawala bora ni msingi wa utendaji wa taasisi za Serikali. Mafunzo haya yatazijengea uwezo taasisi zetu kuwa wazi na kuwajibika. Si kila mtu ana utaalamu wa kila kitu, hata katika bodi zetu kila mmoja ana mchango wake kulingana na uelewa wake,” amesema.
Amesema kupitia mafunzo hayo, Serikali inatarajia mashirika ya umma kuongeza mapato na kuimarisha utoaji wa gawio kwa Serikali.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa CIFA Tanzania, Liz H. Wachuka amesema taasisi hiyo inalenga kuandaa programu zitakazowezesha mashirika ya umma kuelewa wajibu wao katika kudumisha utawala bora.
“Tunaanza kwa kumjengea uwezo mtu mmoja mmoja, kisha taasisi kwa ujumla. Tunaamini mtu asipoweza kujiongoza, hawezi kuwaongoza wengine,” amesema.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa katika taasisi nyingi ni utekelezaji hafifu wa yale yaliyopangwa, hivyo kupitia ushirikiano huo watahakikisha utawala bora unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila mfanyakazi katika mashirika ya umma.
Liz amesema mafunzo wanayotoa ni ya vitendo, yakilenga kuonesha taasisi maeneo ya kuboresha na pale panapohitajika kuanza upya ili kujenga mifumo imara na endelevu ya utawala bora. Andika vichwa vya habari