DODOMA: SERIKALI  kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepunguza kwa kiwango kikubwa ada za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni, ili  kurahisisha uendeshaji wa blogu, Online TV na majukwaa ya kidijitali nchini.

Ada ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni imepunguzwa kutoka Sh 500,000 hadi Sh 50,000, huku ada ya maombi ya leseni ikishushwa kutoka Sh 50,000 hadi Sh 10,000.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji ulioandaliwa na TCRA katika Ukumbi wa New Generation Dodoma , Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha mazingira ya sekta ya habari ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya jamii.

Amesema serikali itaendelea kulinda haki ya wananchi kupata taarifa sahihi na kwa wakati, huku akivitaka vyombo vya habari kuzingatia maadili ya taaluma, kuongeza ubora wa maudhui na kulinda haki miliki.

“Vyombo vya habari vina wajibu wa kuwafikia wananchi wote bila ubaguzi, hususan waliopo vijijini, na kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) ili kuongeza tija,” amesema Mwinjuma.

Katika hatua nyingine, Mwinjuma ameiagiza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha madai ya mishahara na stahiki za wafanyakazi wa vyombo vya habari yanapatiwa ufumbuzi wa haraka, akisema ndani ya wiki moja anatarajia kupokea taarifa ya utekelezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watangazaji Huru Tanzania (NIBA), Amos Ngosha, ameomba Serikali kupunguza idadi ya tozo zinazotozwa sekta ya utangazaji, akieleza kuwa vyombo vya habari hulipa zaidi ya tozo 19 kwa mwaka, jambo linalopunguza uwezo wa kifedha na kuathiri uendelevu wa huduma.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari, amesema mwaka 2025 wanahabari zaidi ya 2,000 walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo, huku usikivu wa redio nchini ukifikia asilimia 85 na usambazaji wa televisheni kupitia satelaiti kufikia asilimia 100.

Ameongeza kuwa hadi Desemba 2025, leseni 770 za utangazaji zilikuwa zimetolewa na  mamlaka hiyo ina mpango wa kuanzisha mfumo wa redio ya kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano.

Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika Februari 12 na 13, 2026, umewakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya utangazaji kujadili mikakati ya kuimarisha na kupanua huduma za habari nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *