
Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa umati mkubwa wa wananchi wa walioshiriki katika maandamano ya kitaifa ya kuadhimisha kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 wametangaza wazi kwamba haki na utu wao haviuzwi.
Araqchi jana alituma chapisho katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X akisema: Katika maandamano ya jana mamilioni ya Wairani kwa mara nyingine tena wametuma ujumbe wa wazi kwa ulimwengu kwamba haki na utu wao haviuzwi.
Ameongeza kuwa umati wa mamilioni ya wananchi walimiminika katika mitaa mbalimbali ya Iran kuadhimisha mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Mapinduzi ya Iran yametajwa na wasomi kuwa “Mapinduzi Makubwa ya Mwisho ya Karne ya 20.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa miongo kadhaa iliyofuata baada ya Mapinduzi ya Kiislamu imeleta maendeleo makubwa, hasa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
“Katika mwaka uliopita pekee, watu wetu wamekabiliwa na shambulio lisilo la kawaida la serikali mbili zenye silaha za nyuklia na kisha operesheni kubwa ya kigaidi; lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa imara kila wakati,”amesisitiza mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.
Israeli ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran mwezi Juni 2025, siku mbili tu kabla ya kufanyika duru ya sita ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani mjini Muscat, Oman. Marekani pia ilijiunga na uchokozi huo na kushambulia vituo vya nyuklia ya Iran.
Wkati huo huo Abbas Araqchi ameeleza matumaini yake kuwa Mwaka Mpya ujao wa Kiirani utakaoanza Machi 21 utaleta amani na utulivu, huku mazungumzo yakiibuka mshindi mkabala wa vita.