
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ametoa mjibizo kwa madai ya Marekani kwamba nchi hiyo ilifanya jaribio la nyuklia mnamo mwaka 2020 na kusisitiza: “Marekani ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha kuvurugika kwa nidhamu ya nyuklia duniani na utulivu wa kimkakati wa kimataifa.”
Lin Jian ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa madai ya Washington kwamba Beijing ilifanya jaribio la nyuklia mwaka 2020 hayana msingi wowote na akabainisha: “kwa kutoa madai kama hayo, Marekani inatafuta njia ya kuhalalisha hatua yake ya kufufua mpango wake wa kufanya majaribio ya nyuklia”.
Aidha, amesema, Marekani imekuwa kila mara ikipotosha na kuitangaza kwa ubaya sera ya nyuklia ya China na akafafanua kwamba: “kwa kweli madai haya ni hatua ya kisiasa ya kudumisha uwezo wa juu wa nyuklia wa Washington na kukwepa kutimiza wajibu wake kupunguza silaha za nyuklia.”
Huko nyuma, Marekani ilishaituhumu Beijing kwamba mnamo mwaka 2020 ilifanya jaribio la nyuklia kwa siri na kutaka uanzishwe mkataba mpya na mpana zaidi wa udhibiti wa silaha ambao mbali na Russia, utaijumuisha China pia.
Tuhuma ambazo Washington ilizitoa katika mkutano wa kimataifa wa upokonyaji silaha zilidhihirisha uwepo wa mvutano mkubwa kati ya Marekani na China katika kipindi nyeti na hasasi kuhusiana na udhibiti wa silaha za nyuklia.
Na hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitangaza kwamba, Mkataba wa New START, unaoweka mipaka ya silaha za nyuklia kwa madola mawili makubwa zaidi duniani yanayomiliki silaha hizo, yaani nchi hiyo na Marekani ulimalizika rasmi tarehe 5 Februari, pasi na kutolewa mjibizo wowote rasmi kutoka kwa Washington kuhusu kuuongezea muda mpya mkataba huo…./