
Uchunguzi uliofanywa na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar umefichua kuwa, utawala wa kizayuni wa Israel umetumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa zenye joto kupindukia katika vita vya mauaji ya kimbari huko Ghaza, na kupelekea “kuyeyuka” maelfu ya miili ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na televisheni hiyo chini ya anuani: Sehemu Iliyosalia ya Kisa (The Rest of the Story), timu za ulinzi wa raia huko Ghaza zilirekodi kesi za Wapalestina wanaokaribia elfu tatu ambao wametoweka tangu vilipoanza vita hivyo vya kinyama Oktoba 2023.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, katika maelfu ya matukio, kilichokuwa kikibaki katika miili ya Wapalestinab baada ya shambulio la jeshi la kizayuni ilikuwa ni vipande vidogovidogo tu vya nyama, chembechembe za damu au hata jivu tupu.
Mbali na vifo vilivyotokana na mashambulio ya viripuzi, yakiwemo makombora na mabomu, wataalamu wa masuala ya kijeshi na mashuhuda wamehusisha pia kile walichokiita ‘kuyeyuka’ kwa Wapalestina kutokana na jeshi la kizayuni kutumia silaha za joto kali kupindukia lilizopatiwa na Marekani, zinazojulikana kama mabomu ya ombwe au erosoli (vacuum or aerosol bombs), zenye uwezo wa kutoa joto linalopindukia nyuzi joto 3,500 Selsiasi.
Msemaji wa shirika la ulinzi wa raia katika Ukanda wa Ghaza Mahmoud Basal aliiambia Al Jazeera kwamba, timu zao zilikuwa zikizingatia idadi ya wakazi katika nyumba na miili inayopatikana baada ya shambulio la jeshi la utawala wa kizayuni.
“Ikiwa familia inatuambia, kulikuwa na watu watano ndani, na tunapata miili mitatu tu kamili iliyosalia, tunawachukulia wawili waliobaki kuwa ‘wameyeyuka’ baada ya utafutaji mkubwa tunaofanya kutoona athari yoyote isipokuwa ya alama za kibiolojia za michirizi ya damu kwenye kuta au vipande vidogovidogo kama vya fuvu la kichwa,” ameeleza Basal.
Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, harakati ya Hamas ilitoa wito kwa kamati ya kimataifa kuchunguza kutumia Israel aina fulani za silaha, ikisisitiza kwamba miili ya Wapalestina inayeyushwa huko Ghaza.
Hadi sasa, jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limeshaua zaidi ya Wapalestina 72,037 na kuangamiza karibu asilimia 90 ya miundombinu ya eneo hilo…/