DAR ES SALAAM: BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekifunga kiwanda cha kutengeneza zege cha JUYE Concrete Company Ltd kilichopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, kufuatia tuhuma za uchafuzi wa mazingira unaowaathiri wakazi wa maeneo jirani.
Zuio hilo limetolewa leo, Februari 12, 2026, na Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamadi Taimuru, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kiwandani hapo kukagua utekelezaji wa maagizo yaliyokuwa yametolewa awali.
Kwa mujibu wa Taimuru, kiwanda hicho kilianza kukaguliwa tangu mwaka jana na kimepewa maelekezo mara nne ili kurekebisha kasoro zilizobainika. Hata hivyo, malalamiko kutoka kwa wakazi wa karibu kuhusu vumbi na maji taka yameendelea kuripotiwa.

Taimuru amesisitiza kuwa ingawa viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, ni lazima viendeshwe kwa kuzingatia ustawi wa wananchi.
“Nchi yetu inahitaji viwanda kwa ajili ya uzalishaji na maendeleo, kwa sababu hakuna maendeleo bila viwanda. Lakini maendeleo haya ni kwa ajili ya watu. Kama kiwanda kinaumiza watu, hata tukizalisha bidhaa hizo hatutakuwa na wa kuwauzia. Ni lazima tulinde afya za wananchi,” amesema Taimuru.
Kutokana na hali hiyo, NEMC imesimamisha uzalishaji katika kiwanda hicho hadi marekebisho yatakapokamilika.
“Tunasimamisha uzalishaji wa kiwanda hiki ili tuwape nafasi ya kufanya marekebisho. Wakikamilisha leo tutakuja kufungua, wakikamilisha kesho watatuarifu na tutakuja,” amesisitiza.

Kwa upande wao, Meneja wa JUYE Concrete Company Ltd, Cao Zhojun, pamoja na msaidizi wake Shery Chen, wamesema wanatambua umuhimu wa kulinda afya ya wananchi na wameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na NEMC ili kurejesha uzalishaji.
Wameeleza kuwa tayari waliagiza vifaa vya ujenzi na walikuwa wamefikia makubaliano na mkandarasi mdogo kuanza kazi za maboresho.
“Tuliagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi na tayari tulikuwa na mkataba na mkandarasi ambaye angeanza kazi. Siku mbili zilizopita tulifikia makubaliano, hivyo kuanzia kesho tutawahimiza waanze kazi mara moja,” wamesema.
Wakati huo huo, NEMC imetembelea kiwanda cha YK Tosh Premix ambacho tayari kilikuwa kimesimamisha uzalishaji kwa hiari ili kufanya maboresho ya kudhibiti vumbi, kelele na majitaka, kufuatia malalamiko ya wakazi wa jirani.

Taimuru amewataka viongozi wa kiwanda hicho kuendelea kusimamisha uzalishaji hadi watakapokamilisha marekebisho na kutimiza matakwa yote ya kimazingira, ikiwemo kupata kibali cha ukaguzi.
Amesisitiza kuwa hata kama ujenzi wa maboresho unaendelea, hautaruhusu kuendelea kwa uzalishaji unaosababisha kero kwa majirani.
Aidha, Taimuru amesema NEMC inatambua umuhimu wa viwanda katika uchumi wa nchi na inaendelea kushirikiana na wawekezaji, lakini ni lazima wazingatie sheria za mazingira ili kulinda afya za wananchi.

Naye, Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Glory Komba, amesema ukaguzi huo ni sehemu ya ufuatiliaji wa maagizo yaliyotolewa awali ili kudhibiti kero kama vumbi, kelele na majitaka kwa wakazi wa maeneo ya jirani.
Amesisitiza kuwa wawekezaji wanapaswa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) kabla ya kuanza miradi yao, ili kupata mwongozo sahihi wa kitaalamu, kupunguza gharama zisizo za lazima na kuepusha usumbufu kwa jamii.
Kwa ujumla, NEMC imeweka wazi kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira ili kuhakikisha maendeleo ya viwanda yanaendana na ustawi wa wananchi.