
Rais Masoud Pezeshkian amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi “katika hamasa ya aina yake” katika maandamano ya kitaifa kote nchini ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Pezeshkian amebainisha haya leo katika mkoa wa Golestan kaskazini mashariki mwa Iran siku moja baada ya mamilioni ya wananchi wa Iran kumiminika mitaani kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu katikati ya vitisho vya karibuni vya Marekani na Israel dhidi ya nchi hii.
Rais wa Iran amesema kuwa “anashukuru sana na kuthamini ushiriki wa aina yake wa wananchi jana Jumatano kote nchini katika maandamano ya madhimisho ya mwaka kwa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu,
Amesema, licha ya mashinikizo na propaganda zote za maadui ili kuwaweka watu mbali na maadhimisho ya jana; wametekeleza juhudi za ziada kwa ajili ya umoja na mshikamano wa nchi.
Akiwa Golestan, Pezeshkian ameongeza kusema: Maafisa wa serikali ya Iran, wabunge na wanasiasa wana jukumu kubwa la kuwatumikia wananchi ambao wamethibitisha kuwa hawawezi kudanganywa.
“Lengo letu ni kutatua matatizo, na hili haliwezekani bila huruma na ushirikiano wa wananchi,” ameeleza Rais wa Iran.
Jana Jumatano wananchi wa Iran kote nchini walishiriki katika maandamano ya kitaifa ya maadhimisho ya mwaka wa 47 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwatolea wito wananchi kushiriki pakubwa katika maadhimisho hayo kwa kudhihirisha irada na istiqama.
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliohudhuria maandamano ya Bahman 22 mjini Tehran jana waliidhinisha azimio la maandamano hayo na kutangaza kwamba, sasa ni wakati wa ushirikiano kati ya medani ya kijeshi na ya diplomasia, na kwamba askari wa nyuga zote hizo mbili wanatokana na kizazi cha taifa na wanaungwa mkono kwa asilimia mia moja na wananchi wa Iran.