
Paul Mackenzie, kiongozi wa tapo la kikristo nchini Kenya aliyewaamuru wafuasi wake wajiue kwa njaa wao na watoto wao ili waende mbinguni amesomewa shtaka jengine jipya yeye na wenzake saba la kusababisha vifo vingine 52, kupitia mahubiri yake.
Mackenzie, ambaye mwaka 2023 aligonga vichwa vya habari baada ya kubainika kuwa alisababisha vifo vya zaidi ya wafuasi wake 400 katika janga lililojulikana kama “Mauaji ya Msitu wa Shakahola”, amekana shtaka hilo jipya alilosomewa jana Jumatano na anandelea kubakia rumande.
Mnamo mwaka jana, miili zaidi iligundulika katika eneo la kijiji cha Binzaro, kilichopo kilomita 30 kutoka msitu wa Shakahola, pembezoni mwa Bahari ya Hindi, ikiashiria kwamba, tapo hilo la Mackenzie lilikuwa lingali likiendelea na ibada zake, hata baada ya yeye mwenyewe kukamatwa.
Kupitia taarifa yake iliyowekwa kwenye ukurasa wa X, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka nchini Kenya ilisema, imemshitaki Mackenzie na wenzake kwa kosa la kufanikisha vitendo vya kigaidi, kutokana na vifo vya watu wa 52, katika eneo la Kwa Binzaro, Kaunti ya Kilifi.
Washitakiwa hao walikana makosa hayo, na kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Machi 4, mwaka huu.
“Wanatuhumiwa kwa kueneza imani hii ya kikatili ambayo imefanikisha vitendo vya kigaidi,” ilieleza taarifa ya ofisi hiyo ya Mwenedesha Mashtaka wa Serikali ya Kenya.
Mackenzie alijipatia umaarufu kwa kuwahubiria waumini wake washinde njaa, na baada ya kufa wakutane na Yesu…/