Chanzo cha picha, Anadolu Via Getty
Baada ya kukutana na Benjamin Netanyahu, Donald Trump aliandika kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii la Truth:
“Hakuna matokeo ya uhakika yaliyopatikana, isipokuwa nilisisitiza kuwa mazungumzo na Iran yanaendelea kuona ikiwa makubaliano yanaweza kufikiwa.” Bw. Trump pia aliandika: “Nilimfahamisha Waziri Mkuu [Netanyahu] kwamba mapendeleo yetu ni makubaliano.
Tutaona matokeo yatakuwaje. Mara ya mwisho Iran iliamua kutoshughulika na ikashambuliwa kupitia [Operesheni] Midnight Hammer. Natumai watachukua hatua kwa busara na kuwajibika zaidi wakati huu.” Bw.Trump pia aliandika kwamba amezungumza pia masuala ya Gaza na Waziri Mkuu wa Israel.
“Tulijadili maendeleo makubwa ambayo yamepatikana huko Gaza na kanda kwa ujumla,” aliandika. Baada ya kikao hicho, ofisi ya Benjamin Netanyahu pia ilitangaza kuwa Waziri Mkuu wa Israel alisisitiza katika kikao hicho kwamba katika mazungumzo ya Marekani na Iran, kipaumbele chake ni kuhakikisha usalama wa Israel.
Kwa mujibu wa AFP, Bw. Netanyahu alikubaliana na Rais wa Marekani “kuratibu na kuwasiliana” ili kuendeleza mazungumzo ya Iran na Marekani.
Bw. Netanyahu alikutana na Steve Whittaker, mjumbe maalum wa Donald Trump, na Jared Kushner, mkwe wa Bw. Trump, jana usiku baada ya kuwasili Washington.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, wawili hao “walishiriki ripoti na Netanyahu kuhusu duru ya kwanza ya mazungumzo na Iran Ijumaa iliyopita.”