Chanzo cha picha, Noel Ebrin Brou/BBC
-
- Author, Nicolas Négoce
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Nioronigué
- Author, Abayomi Adisa
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Lagos
-
Muda wa kusoma: Dakika 4
Tahadhari: Taarifa hii ina maelezo ambayo huenda yakawaathiri baadhi ya wasomaji
Yameogo Aminata, 57, bado ana anahangaika na kumbukumbu za matukio yaliyosababisha mauaji ya wanawe wanne yaliyofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali za kidini nchi mwake, Burkina Faso. Ameisimulia matukio hayo akiwa ameketi katika chumba chenye giza kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ivory Coast,
Mnamo mwaka wa 2022, alikuwa mbali na nyumba yake wakati waasi wenye silaha – ambao wamekuwa wakihangaisha jamii za katikati mwa Burkina Faso kwa karibu miaka 15 – walipowavamia.
Wanamgambo wa kijihadi walikuwa wameteka kijiji chao, wachukua ng’ombe na ardhi, na kuua wakaazi wengi – ikiwa ni pamoja na wanawe walio umri wa kati ya 25 na 32.
“Waliwachinja watoto wangu wanne,” aliambia BBC, mwili wake ukitetemeka huku hisia zikimzidi.
“Nilipofika, walikuwa wakimuua mwanangu wa nne.”
Aminata anasema alichukua kisu ili kupambana naye, lakini alizidiwa nguvu, akapigwa na kutupwa porini na kuachwa na majeraha makubwa kichwani, begani na kooni.
Anasema alitenganishwa na binti yake wakati wa shambulio hilo, na hawajawahi kumuona tangu wakati huo.
Mnamo 2023, Aminata alikimbilia kambi ya wakimbizi ya Nioronigué katika nchi jirani ya Ivory Coast, akiweka nguo zilizokuwa na damu kutoka siku hiyo kama ukumbusho wa madhila aliyopitia.
“Sijui jinsi ya kuendelea na maisha yangu. Sina chochote,” aliiambia BBC.
Takriban watu 10,000 wameuawa katika uasi nchini Burkina Faso, ambao pia umezikumba nchi jirani za Mali na Niger.
Umoja wa Mataifa umelitaja eneo hilo kama “kitovu” chamashambulizi ya kimataifa ya wanamgambo wenye itikadi kali.
Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Wanajeshi walichukua mamlaka katika nchi zote tatu, na kuahidi kukabilian na uasi.
Wametengana na washirika wao wa jadi huko Magharibi, na kugeukia Urusi kwa msaada wa kijeshi.
Ingawa vikosi vya Urusi, vinavyohudumu chini ya shika lake la ulinzi la wa Africa Corps, vimepelekwa nchini Burkina Faso, mashambulizi ya wanamgambo yamezidi kuongezeka, kundi linalowahangaisha zaidi likiwa ni Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) ambalo lina mafungamano na al-Qaeda.
Kama na Aminata, Hassane Tall, 60, ambaye alikimbia kaskazini mwa Burkina Faso 2023 pamoja na wake zake watatu na watoto 19 baada ya kukabiliwa na mashambulio kadhaa.
“Tulitoroka makabiliano kati ya makundi ya kijihadi na vikosi vya usalama,” alisema. “Tulifikiri tungelikufa.”
Tall ambaye sasa anaishi katika kambi ya Nioronigué, anasema kuwa kuacha ardhi ya mababu zake kulimuumiza sana, lakini hana matumaini ya kururudi nyumbani kwa familia yake.
Kambi ya Nioronigué ambayo imejengwa katika ardhi ya hekari 12 inawahifadhi Aminata na Tall iko karibu na mpaka wa Burkina Faso. Ilianzishwa mwaka na UN na mamlaka za Ivory Coast mwaka 2023.
Kambi hii ambayo ina uwezo wa kuwahifadhi watu takriban 6,000, na nyingine iliyo karibu Timala sasa ina wakimbizi karibu 13,000 – idadi ambayo inazidi kiwango kinachohitajika.
Data ya Umoja wa Mtaifa inaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni tatu wamefurushwa makwaokutokana na mizozo tofauti katika eneo la Sahel region.
Zaidi ya watu 80,000 kutoka Burkina Faso sasa wanaishi katika kambi ya wakimbizi nchini Ivory Coast.
Akishukuru kwa kupewa makaazi, Aminata alisema: “Naishukuru Ivory Coast, na raia wake wote.”
“Niliondoka nyumbani kwangu kwa sababu tulifurushwa na wanamgambo wenye itikadi kali. Walisema wanataka nchi,” aliongeza.
Chanzo cha picha, Noel Ebrin Brou/BBC
Simulizi na watu kupoteza wapendwa wao msongo wa mawazo uliotokana na madhila hayo zimeenea kila mahali katika kambi hiyo.
Baadhi ya wakimbizi wanatokea Mali. Wanajumuisha mhitimu wa masuala ya fedha mwenye umri wa miaka 27. Yeye na kaka zake hivi majuzi walisafiri kwa mashua ya mbao chini ya Mto Niger huko Gao kaskazini mwa Mali hadi mji mkuu, Bamako, kisha wakaabiri basi kuelekea kaskazini mwa Ivory Coast kukimbilia usalama.
Mhitimu huyo alisema walilazimika kuondoka baada ya binamu yao mwenye umri wa miaka 24 kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi.
“Alikuwa mvuvi, alikuwa akitoka kuvua samaki usiku kama kawaida yake, alivamiwa na watu wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki, haya ni mambo yanayotokea kila siku.
“Tulikuwa tunaishi kwa hofu, bila kujua kama tutaamka siku iliyofuata,” aliambia BBC.
Uchumi wa Ivory Coast ni moja wapo ya nchi zinazokua kwa kasi katika eneo hilo, lakini ukosefu wa ajira na umaskini umesalia kuwa juu, huku wenyeji katika maeneo ya mpakani wakiwa na wasiwasi kuhusu wimbi la wakimbizi.
Lakini mwakilishi wa serikali Djamatigui Touré aliambia BBC kwamba wakimbizi hawatarudishwa nyuma.
“Wale wanaokuja ni ndugu zetu; historia na utamaduni ni sawa,” alisema.
Hata hivyo, mwakilishi mkazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, Blerta Cela, alionya kuwa hali ya kibinadamou inaendelea kuwa tete..
“Idadi ya wakimbizi imeongezeka sana. Wengi wao hawako katika kambi. Wanahifadhiwa na familia za Ivory Coast,” alisema..
Kwa Aminata, kuanza maisha upya katika nchi nyingine kunazua kumbukumbu ya matukio aliyoacha nyuma.
“Nimeshindwa kusahau kile kilichonikuta,” anasema.
“Tunamuomba Mungu amani ipatikane Burkina Faso.”
Taarifa ya ziada na Noel Ebrin Brou