Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ametoa wito wa kuwepo Afrika yenye nguvu na mshikamano zaidi ili kulilinda bara hilo dhidi ya ‘hatua za unyanyasaji’ na ukandamizaji za pande za kigeni.

Gedion Timothewos ameeleza haya katika kikao cha kawaida cha 48 cha Baraza  la Utendaji la Umoja wa Afrika (AU) katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Akihutubia wajumbe wa kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia amesisitiza kuwa  umoja wa Afrika unapasa kuwa wa kweli ikiwa bara hilo linataka kulinda maslahi yake katika mazingira tata ya sasa duniani, ambapo ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi unazongwa na masuala ya kisiasa na kiusalama.

Gedion ameongeza kuwa Afrika inahitaji “si hisani tu au nia njema ya wengine bali ushirikiano wa kweli ambao unategemea nguvu zinazotokana na kuwepo umoja na mshikamano.” 

Amezungumzia pia mashinikizo ya ndani akieleza kuwa kuingia madarakani serikali kinyume na katiba katika nchi kadhaa za Afrika kunaendelea kubomoa misingi ya  Umoja wa Afrika na kudhoofisha amani na usalama katika bara zima.

Mawaziri wa Mambo ya Nje barani Afrika wanakutana Addis Ababa kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) uliopangwa kufanyika Februari 14-15.

Ukumbi wa mikutano wa AU, Addis Ababa

Mkutano wa mwaka huu utafanyika chini ya mada “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo ya Usafi wa Mazingira Ili Kufikia Malengo ya Ajenda ya 2063.”

Majadiliano katika Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika yanatarajiwa kubuni rasimu ya maamuzi yatakayozingatiwa na wakuu wa nchi, ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya marekebisho ya uongozi, ushirikiano wa kiuchumi na uwakilishi wa Afrika katika taasisi za kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *