MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Balozi Simon Sirro ametembelea baadhi ya miradi ya shirika hilo na kueleza kufurahishwa na utendaji na usimamizi mzuri.
Aidha Balozi Sirro amekiri kuridhishwa na maendeleo ya uendeshaji wa Mgodi wa Madini ya Dhahabu wa Buckreef (BGC) unaomilikiwa na STAMICO kwa asilimia 45 huku asilimia 55 zikimilikiwa na mbia.
Balozi Sirro ametoa pongezi hizo alipofanya ziara yake mkoani Geita na kukagua Kituo cha Mfano cha STAMICO kilichopo kata ya Lwamugasa na Mgodi wa Bucreef uliopo kata ya Busanda wilayani Geita.

Amesema pamoja na kazi nzuri inayofanyika ni muhimu kutambua kuwa ili malengo ya uwekezaji STAMICO yaweze kufikiwa, kila mtendaji anao wajibu wa kusimamia weledi na uadirifu kwenye nafasi yake.
Balozi Sirro amesema mtumishi yeyote asiyejituma na kufanya kazi kwa ufanisi hana nafasi kwa kuwa Serikali imejizatiti kulinda uhai wa Shirika kwa maslahi mapana ya Taifa kwani STAMICO ni mali ya Watanzania.
Amesisitiza matarajio ya Serikali ni kuona STAMICO na Buckreef zinajiendesha kwa faida na kuongeza mchango katika pato la Taifa na hivyo ni vyema wasimamie weledi na uadilifu katika uendeshaji wa mradi huo.
Balozi Sirro pia amefurahishwa kuona miradi ya shirika inaendeshwa na Watanzania na ameelekeza uwajibikaji uliotukuka kwa watendaji wote wa STAMICO ili kuendelea kuliweka Shirika katika soko la ushindani kwenye sekta ya madini.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala amesema kwa kutambua mwitikio wa wachimbaji wadogo kupata huduma za uchenjuaji katika vituo vya mfano, shirika limejizatiti kuongeza vituo zaidi vya mfano.
Amesema ili kupanua uwigo wa fursa, STAMICO imejipanga kufanya uwekezaji wa vituo vya uchakataji na uchejuaji kwenye mikoa tofauti inayozalisha kwa wingi aina nyingine ya madini tofauti na dhahabu.
Msimamizi wa Kituo cha mfano cha STAMICO cha Lwamugasa-Geita, Victor Augustine amesema usimamizi thabiti wa kituo umekifanya kuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo na kuchangia pato sh bilioni 1.9 tangu mwaka 2020.
Naye, Meneja Mkuu wa Buckreef, Isaac Bisansaba amesema mgodi umewekeza takribani sh bilioni 230 na unazalisha wastani wa kilo 62 za dhahabu kwa mwezi ambapo ameahidi kuwa wapo tayari kushirikiana na STAMICO kuongeza uzalishaji.