
Wajumbe wamepokea taarifa kutoka kwa Naibu Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Claudio Cordone, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ufadhili na Ushirikiano katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA.
UN yataka utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano
Akilihutubia Baraza hilo Bwana Claudio Cordone amekaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano ya Januari 30 kati ya Serikali ya Mpito ya Syria na Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria, akiyataja kama hatua muhimu ya kupunguza mvutano.
Makubaliano hayo yanatoa mwongozo wa mchakato wa utaratibu wa ujumuishaji wa kijeshi na kiutawala, pamoja na masharti yanayohusu kurejea kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao na kulinda haki za kiraia na kielimu za Wakurdi wa Syria.
“Hadi sasa, mapigano yamesitishwa na maandalizi ya mpango wa utekelezaji yanaendelea kwa njia chanya,” amesema Bwana. Cordone.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa hatua inayofuata ni ya msingi sana.
“Tunasubiri kwa matarajio makubwa utekelezaji wake kamili na wa haraka, hususan kuhusu ujumuishaji wa amani wa kaskazini-mashariki mwa Syria, ulinzi wa haki za Wakurdi wa Syria, na kurejea salama, kwa hiari na kwa heshima kwa watu waliokimbia makazi yao,” ameongeza.
Majadiliano ya Baraza la Usalama pia yamelenga athari za kibinadamu za mapigano yanayoendelea kaskazini mwa Syria na madhara yake kwa uthabiti wa eneo hilo.
Licha ya jitihada, mahitaji ya kibinadamu bado ni makubwa
Pamoja na ishara za utulivu katika baadhi ya maeneo, maafisa wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa kiwango cha mateso nchini Syria bado ni kikubwa.
“Zaidi ya watu milioni saba wanakabiliwa na uhaba mkubwa au wa wastani wa chakula,” amesema Mkurugenzi wa Idara ya Ufadhili na Ushirikiano katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura OCHA.
Amesisitiza kuwa kwa kuboresha hali kwa muda mrefu, kunahitajika uwekezaji mkubwa na wa kulengwa katika ujenzi mpya na maendeleo. Hata hivyo, kwa sasa, ufadhili wa misaada ya kibinadamu unabaki kuwa wa lazima.
“Mwaka 2025, licha ya kupungua kwa asilimia 36 ya rasilimali, tuliweza kuwasaidia watu milioni 3.8 kila mwezi. Hili ni ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka uliopita,” amebainisha.
Ameongeza kuwa kwa rasilimali zaidi, Umoja wa Mataifa utaweza kupanua msaada kwa mamilioni ya watu zaidi.
“Tuna fursa adimu ya kuisaidia watu wa Syria kujinasua kutoka katika moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuitumia fursa hii.”
Syria katika njia panda na wakati muhimu
Mkutano wa Baraza la Usalama umeonesha kuwa Syria ipo katika wakati nyeti. Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yanatoa matumaini ya kuelekea utulivu na maridhiano, mahitaji ya kibinadamu bado ni makubwa sana.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameweka wazi kuwa dhamira ya kisiasa endelevu pamoja na ufadhili wa kutosha wa misaada ya kibinadamu vitakuwa muhimu katika kuamua kama taifa hilo litaweza kusonga mbele kutoka katika usitishaji wa mapigano ulio dhaifu kuelekea amani ya kudumu na ujenzi upya.