Dar es Salaam. Mkazi wa Kigamboni, Abdul Chusi na mkewe Mwanaidi Omary, mwishoni mwa wiki hii watakuwa wakisherehekea Siku ya Wapendanao visiwani Zanzibar baada ya kujishindia safari ya kimahaba ya Valentine iliyoandaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Halotel Tanzania.

Chusi ametangazwa Ijumaa, Februari 13, 2026 kuwa mshindi wa safari hiyo ya wikiendi ya wapendanao kupitia kampeni maalum ya Valentine iliyowashirikisha wateja wa Halotel katika majukwaa mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kumtangaza mshindi, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Halotel, Shabani Said amesema lengo la kampuni hiyo si tu kutoa huduma nafuu na za kuaminika za mawasiliano, bali pia kuunganisha watu kupitia programu zenye kugusa hisia na kuleta athari chanya kwa jamii.

Amesema kampeni hiyo iliwahamasisha wateja kushiriki hadithi zao za mapenzi na kusherehekea mahusiano yenye maana.
“Katika Halotel tunaamini upendo ni muunganiko. Msimu huu wa Valentine tulitaka kwenda zaidi ya huduma zetu za mtandao na kuunda uzoefu utakaokumbukwa milele na wateja wetu. Tunajivunia kuifanya hafla hii kuwa ya kipekee kwa washindi wetu,” amesema Said.

Ameongeza kuwa safari hiyo ya Zanzibar imejumuisha malazi ya kifahari, chakula cha jioni cha kimahaba na shughuli mbalimbali maalum kwa ajili ya wenzi hao ili kuwapatia kumbukumbu isiyosahaulika ya kusherehekea upendo wao.

Kwa upande wake, Chusi amesema amefurahi kushinda zawadi hiyo akisema awali hakuamini alipopigiwa simu kumtaarifu ushindi wake.
“Nilipopigiwa simu sikuamini. Baadaye walipopiga tena nikamtaarifu mke wangu, lakini hata yeye hakuamini hadi tulipofika ofisini kwa Halotel na kupokelewa ndipo tukathibitisha,” amesema.

Naye Mwanaidi Omary amewahimiza wananchi kushiriki kampeni za kampuni hiyo ili kujiongezea nafasi ya kujishindia zawadi.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Halotel, Roxana Kadio amesema kampeni hiyo ya Valentine imelenga kuthamini na kuwazawadia wateja waaminifu kwa kuwapatia uzoefu halisi na wa thamani unaozidi huduma za mawasiliano.
“Baada ya kujishindia safari ya kwenda Zanzibar, Bwana na Bi Chusi watasherehekea siku hiyo wakiwa huko kwa pakeji maalum tuliyowaandalia ili wafurahie kikamilifu safari yao ya wapendanao,” amesema Kadio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *