Zanzibar. Benki ya Exim Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kukuza sekta ya utalii nchini baada ya kudhamini mkutano wa Z-Summit 2026 kama mdhamini  mkuu, hafla iliyofanyika Februari 11–12 katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Tunguu.

Hii ni mara ya nne mfululizo kwa benki hiyo kudhamini mkutano huo tangu kuanzishwa kwake, jukwaa linalowakutanisha wawekezaji wa utalii, waendeshaji wa safari, wamiliki wa hoteli, mawakala wa usafiri na watunga sera kutoka Tanzania na nje ya nchi kujadili fursa na mwelekeo wa maendeleo endelevu ya utalii Zanzibar.

Kupitia ushiriki wake, Exim imeendelea kuonesha suluhisho za kifedha na kidijitali zinazolenga kuongeza ufanisi wa biashara za utalii, ikiwemo akaunti maalum kwa waendeshaji wa utalii, huduma za bima na mifumo ya malipo ya kielektroniki.

Benki hiyo pia ilikuwa ya kwanza nchini kuzindua Kadi ya Exim TANAPA inayowawezesha waendeshaji wa utalii kufanya malipo ya viingilio vya hifadhi kwa njia ya kielektroniki.

Mfumo huo sasa umeboreshwa na kuruhusu malipo moja kwa moja kutoka akaunti za waendeshaji kwenda TANAPA na NCAA kupitia majukwaa ya mtandaoni, hatua inayoongeza ufanisi na kupunguza muda wa miamala.

Mbali na hilo, Exim imeimarisha mnyororo wa thamani wa utalii kwa kutoa mikopo ya muda mfupi kwa wasambazaji wa bidhaa na huduma katika ekolojia ya sekta hiyo kupitia mfumo wa kidijitali usiohitaji dhamana ya ziada, jambo linalosaidia kuboresha mtiririko wa fedha na uendeshaji wa biashara.

Ikiendana na mkakati wake wa kupanua huduma, benki hiyo imetangaza mpango wa kufungua tawi jipya Paje, Zanzibar, ili kusogeza huduma za kifedha karibu na wadau wa utalii, wajasiriamali na jamii.

Akizungumza kwa niaba ya benki, Ofisa Mkuu wa Fedha, Shani Kinswaga, amesema upanuzi huo utaimarisha mchango wa benki katika kukuza utalii kama injini ya uchumi wa Zanzibar.

“Kwa kusogeza huduma za kifedha karibu na waendeshaji wa utalii, wajasiriamali na jamii zinazozunguka, tunaboresha ujumuishaji wa kifedha na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi unaotegemea utalii Zanzibar,” amesema Kinswaga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Mohammed, ameipongeza Benki ya Exim kwa kuendelea kushirikiana na sekta ya utalii, akisema upatikanaji wa huduma za kifedha ni muhimu kwa uendelevu wa sekta hiyo.

Amesema dhamira ya benki kupanua huduma visiwani itaongeza imani kwa wawekezaji na waendeshaji wa utalii, huku ikichochea ukuaji wa biashara na ajira Zanzibar.

Kwa kudhamini Z-Summit 2026 na kupanua huduma zake visiwani, Benki ya Exim inaendelea kujipambanua kama mshirika wa kimkakati wa sekta ya utalii na mchangiaji wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *