Chanzo cha picha, KCNA Via Reuters
Muda wa kusoma: Dakika 4
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amemchagua binti yake kuwa mrithi wake, shirika la ujasusi la Korea Kusini liliwaambia wabunge siku ya Alhamisi.
Ni machache sana yanayojulikana kuhusu Kim Ju Ae, ambaye katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akipigwa picha pamoja na baba yake katika matukio maarufu kama vile ziara ya Beijing mnamo mwezi Septemba – safari yake ya kwanza inayojulikana nje ya nchi.
Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) ilisema ilizingatia “mambo mbalimbali” ikiwa ni pamoja na uwepo wake unaozidi kuwa maarufu hadharani katika matukio rasmi” katika kufanya tathmini hii.
NIS pia ilisema itafuatilia kwa karibu kama atahudhuria mkutano mkuu wa chama cha Kaskazini baadaye mwezi huu – tukio kubwa zaidi la kisiasa ambalo hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano.
Chama tawala ndio chenye kutarajiwa kutoa maelezo zaidi kuhusu vipaumbele kama vile sera za kigeni, mipango ya vita na matarajio ya nyuklia kwa miaka mitano ijayo.
Siku ya Alhamisi mbunge Lee Seong-kwen aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ju Ae, ambaye hapo awali alielezewa na NIS kama “anayefunzwa” kuwa mrithi, sasa alikuwa katika hatua ya “uteuzi wa mrithi”.
Kulingana na shirika la kijasusi la Korea Kusini, Ju Ae ndiye anayetarajiwa kuwa mrithi wa babake.
Chanzo cha picha, KCNA
Ju Ae, anaaminika kuwa mtoto wa pili wa Kim Jong Un na mke wake, Ri Sol-Ju, wakiwa na watoto watatu. Hata hivyo Kim ni msiri sana kuhusu familia yake, alimtambulisha mkewe kwa umma baada ya muda mrefu kupita tangu kuoana.
Kim Ju Ae ndiye mtoto wao pekee ambaye kuwepo kwake kumethibitishwa na uongozi wa nchi hiyo. Hakuna mtoto mwingine ambaye ameonekana hadharani.
Habari za kuwepo kwake ziliibuka kwa mara ya kwanza kutoka kwa mchezaji wa mpira wa vikapu Dennis Rodman, ambaye alifichua kwa gazeti la The Guardian mwaka 2013 kwamba “alimbeba mtoto Ju Ae” wakati wa safari ya kwenda katika nchi hiyo.
Kim Ju Ae
Chanzo cha picha, KCNA
Hakukuwa na taarifa nyingi kuhusu binti huyo hadi Novemba 2022, alipoonekana pamoja na baba yake wakati wa uzinduzi wa kombora la masafa marefu (ICBM).
Februari mwaka uliofuata, alikuwa akionekana mara kwa mara na kuhudhuria karamu za maafisa wakuu.
Shirika la Kitaifa la Ujasusi la Korea Kusini (NIS) lilitoa maelezo machache kwa wabunge kuhusu msichana huyo, kulingana na shirika la habari la AP.
Shirika hilo lilisema binti huyo anapanda farasi, kuteleza kwenye theluji na kuogelea, na alisomeshwa nyumbani katika mji mkuu Pyongyang. Na ana umri wa miaka 10.
Kufikia Januari 2024, NIS lilitoa taarifa nyingine: msichana huyo ndiye “mwenye uwezekano mkubwa” wa kumrithi Kim Jong Un – ingawa walibaini kuwa bado kuna uwezekano wa kurithi nafasi nyingine kwa sababu baba yake bado ni mdogo.
Tangu wakati huo, ameonekana kando ya baba yake mara nyingi. Akiwa amesimama karibu naye katika uzinduzi wa ICBM na gwaride la kijeshi, amepokea saluti za kijeshi kutoka kwa makamanda wakuu wa kijeshi.
Chanzo cha picha, KCNA
Lakini Jumanne ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana nje ya Korea Kaskazini, na safari hiyo huenda ikachochea zaidi uvumi kuwa huenda akamrithi babake.
Familia ya Kim, ambayo imetawala Korea Kaskazini tangu 1948, inawaambia raia wa nchi hiyo kuwa familia hiyo inatoka kwenye damu takatifu, kumaanisha wao pekee ndio wanaweza kuongoza nchi.
Hata hivyo, kuna uvumi kwamba Kim amemtambulisha binti yake katika hatua hii ili kujaribu kuondokana na chuki katika nchi yenye mfumo dume, ambayo haijawahi kuongozwa na mwanamke.
Kuna uwezekano akawa mrithi?
Korea Kaskazini imejitenga sana na haijulikani kwa ulimwengu wa na wengi wanajiuliza kwanini kuonekana kwa Kim Ju Ae karibu na baba yake imekuwa mara kwa mara.
Raia wa Korea Kaskazini wanaambiwa kuwa Kims anatoka kwenye damu takatifu, ikimaanisha tu hao ndio watu wanaweza kuongoza nchi na baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kumtambulisha kwa umma katika umri mdogo kama huo inaweza kuwa njia ya kiongozi wa Korea Kaskazini ya kuhakikisha kuwa binti yake anajiimarisha muda mrefu kabla ya kuchukua madaraka.
Hakuna pendekezo kwamba huenda kurithishwa kwake mamlaka kukatokea wakati wowote hivi karibuni, na uvumi wa zamani kwamba Kim Jong Un alikuwa katika hali mbaya ya afya umetupiliwa mbali.