
NAIROBI – Serikali ya Kenya inaunga mkono kuahirishwa kwa mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Afrika mwaka ujao, ambapo Kenya, Uganda na Tanzania wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Jarida la The Guardian limemnukuu mwenyekiti mwenza wa matayarisho ya mashindano hayo, Nicholas Musonye, kwamba Kenya inaunga mkono kuahirishwa kwa mashindano hayo hadi mwaka 2028, kutokana na uwezekano wa kutokea kwa vurugu za uchaguzi kipindi cha mashindano, ambapo Kenya pia itakuwa inashiriki uchaguzi mkuu, kipindi hiki wawakilishi kutoka CAF wakizuru Tanzania kutathmini hatua zilizopigwa kwa matayarisho.
Musonye ametolea mfano chaguzi za Tanzania na Uganda na kusema hiyo ni ishara tosha kuwa huenda uchaguzi wa Kenya pia ukagubikwa na vurugu wakati wa mashindano hayo.
Hata hivyo, huenda mashindano hayo yasiahirishwe kutokana na kwamba ratiba ya mashindano ya mwaka 2028 tayari imepangwa.
Rais wa CAF, Patrice Motsepe, ambaye amezuru Kenya mara kadhaa, amekuwa akieleza imani yake kuwa mashindano hayo yatafanyika.
Kenya imekuwa ikishuhudia vurugu za baada ya uchaguzi hasa mwaka 2007 na 2017. Ni miaka miwili iliyopita raia kadhaa waliuawa wakati wa maandamano ya vijana.