MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dk. Emmanuel Lameck Mkilia, amesisitiza kuwa kutotekeleza matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPA) ni hatari kubwa kwa faragha, usalama na haki za wananchi.
Akifungua mafunzo maalum kwa maafisa ulinzi wa taarifa binafsi awamu ya saba, yaliyoandaliwa yaliyofanyika jijini Mbeya, Dk. Mkilia amesema baadhi ya taasisi bado hazijatekeleza kikamilifu masharti ya PDPA, hususan katika usajili na uteuzi wa Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na baadhi ya taasisi zinaendelea kukusanya na kuchakata taarifa binafsi bila kufuata matakwa ya kisheria.
“Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi unafanyika kwa kuzingatia kikamilifu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi. Tunatarajia kuona mabadiliko ya vitendo katika taasisi zinazoshiriki,” amesema Dkt. Mkilia.
Ameongeza kuwa PDPC imejipanga kuanza ukaguzi wa utekelezaji wa sheria, kufuatilia usajili na uteuzi wa Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na kuchukua hatua za kisheria pale kutabainika ukiukwaji. SOMA: Matukio mwaka 2024; Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi yazinduliwa
