IMEELEZWA kuwa baadhi ya redio zilizoanzishwa nchini zimekufa kutokana na mitaji midogo na kukosekana kwa menejimenti nzuri ya mapato ya taasisi hizo.

Haya yameelezwa jijini Dodoma na Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Andrew Kisaka wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vya utangazaji.

Alisema kwa sasa kuna baadhi ya vyombo vya habari vya utangazaji ambavyo zinafanya vizuri lakini kuna vingine vinakufa kutokana na mitaji midogo.

“Kuna redio ambazo zinafanya vizuri na hizi zinahitaji kuwekewa mazingira ili ziendelee kuwepo, lakini kuna ambazo zimekufa kutokana na sababu kadhaa hikiwemo mitaji midogo, walioanzisha hawakuwa wanaiwelewa biashara.

“Pia kunakukosekana kwa menejimenti ya rasimali fedha utakuta mmiliki ana biashara sita, hela za huku zinaenda kule au anakuja na kusema nipe laki mbili hivi vinachangia kufa kwa vyombo vya utangazaji, lakini pia uchumi wa nchi unamchango wake katika hili,” amesema.

Awali akiwasilisha mada, Kisaka alibainisha mapendekezo ya Matokeo na Utekelezaji wa Mapendekezo yatokanayo na Utafiti wa Huduma za Utangazaji nchini kuwa ni kurahisisha suala la leseni kwa kuwa na leseni ya maudhui na miundombinu na muda wa leseni uongezeke kutoka miaka mitano hadi miaka 10 na kupunguza gharama za leseni.

Pia wamependekeza kuondolewa mipaka ya kuwa na vyombo utangazaji vya mikoa au vijijini kwa upande wa redio na kwa online kutakuwa na vyombo chipukizi ambavyo vitafanya kazi kwa mwaka mmoja bila kulipa ada.

Mkutano huo unashirikisha wadau wa utangazaji kutoka vyombo vya televisheni, redio na mitandano ya kijamii.

Katika siku ya pili ya mkutano huo, wabobezi katika utangazaji watawasilisha mada za Nafasi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote katika kuwezesha utangazaji vijijini na mawasiliano ya serikali katika zama za kidigitali katika kuimarisha ufikishaji wa taarifa vijijini.

Pia kuna wasilisho la Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde katika kuandaa na kusimamia maudhu ina umuhimu wa ithibati kwa watangazaji na waandishi wa habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *