Msiendekeze sangoma, pimeni afyaMsiendekeze sangoma, pimeni afya

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amehimiza Watanzania waripoti changamoto za kiafya mapema ili kupata huduma stahiki badala ya kuendekeza waganga wa kienyeji. Dk Mwigulu amesema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la Kimataifa la Kisayansi la Saratani na maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dar es Salaam.

Ameiagiza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na sekta binafsi ihamasishe na kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu matumizi mabaya ya tumbaku na pombe kali ambavyo ni visababishi vya saratani ili kusaidia kupambana na ugonjwa huo. SOMA: Dk Mwigulu ataka ushirikiano wa kikanda mapambano dhidi ya saratani

Dk Mwigulu amesema ili kufanikiwa katika harakati za mapambano dhidi ya saratani Wizara ya Afya na wadau wa sekta ya afya wanapaswa kuongeza bidii katika tafiti za kisayansi ili kuangamiza saratani na kwamba tafiti hizo zitumike vizuri badala ya kuziweka kwenye makabati.

Aidha, amesema serikali imefanya uwekezaji mkubwa wenye thamani ya Sh bilioni 18.5 kwa kuanzisha huduma ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa kimatibabu vinavyounganisha picha za utendaji kazi wa mwili (PET) na picha za muundo wa mwili (CT) ili kugundua saratani mapema, kubaini hatua yake na kufuatilia matibabu (PET-CT scan) pamoja na mashine ya Cyclotron.

Sambamba na hayo, amebainisha kuwa lengo la kufanya uwekezaji mkubwa namna hiyo ni kupunguza vifo vitokanavyo na saratani kwa angalau asilimia 30 ifikapo mwaka 2030. Aidha, alisema katika hali ya kawaida, Bara la Afrika haliwezi kushinda vita dhidi ya ugonjwa wa saratani ikiwa kila nchi itafanya kazi peke yake.

Amesema ili kufikia malengo ya mapambano dhidi ya saratani, kunahitajika kuwepo kwa ushirikiano wa kikanda na wa bara zima katika utafiti, mafunzo, kubadilishana wataalamu na kubadilishana rasilimali, teknolojia na uzoefu. “Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi zote za Afrika na kupitia Taasisi ya Saratani Ocean Road tutaendelea kuwa kituo cha ushirikiano wa kikanda na bara zima katika mapambano dhidi ya saratani,” alieleza Dk Mwigulu.

Amesisitiza kuwa kupitia simulizi za machapisho ya kitafiti na sayansi ambazo wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road na Tanzania kwa ujumla wameyafanya, yamekuwa na mchango mkubwa ndani na nje ya nchi kisera na kiutendaji katika mapambano dhidi ya saratani.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya kuandaa mkakati madhubuti wa kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa saratani ili kupunguza athari kwa rasilimaliwatu, uchumi na ustawi wa taifa kwa ujumla. “Kutokana na tahadhari ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani kuhusu ugonjwa wa saratani kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030, Wizara ya Afya mnapaswa kuandaa mikakati ya kupunguza idadi ya wagonjwa wapya,” alisisitiza.

Amesema serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa saratani kwa ustawi wa nguvu kazi ya Watanzania, imeendelea kuchukua hatua ikiwamo kuweka mifumo mizuri ya kisera, kutekeleza mipango na mikakati muhimu dhidi ya ugonjwa huo. “Serikali kwa kutambua athari za ugonjwa wa saratani kwa ustawi wa nguvukazi ya Watanzania imeimarisha wigo wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani za aina mbalimbali ikiwemo saratani ya mlango wa kizazi, matiti, tezi dume na utumbo hadi katika ngazi ya msingi,” aliongeza Dk Mwigulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *