
Dar es Salaam. Ligi Kuu Bara inaendelea tena leo kwa mechi mbili kupigwa, ambapo maafande wa JKT Tanzania itakuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuikaribisha Coastal Union, huku Mtibwa Sugar ikipambana dhidi ya maafande wa Mashujaa.
JKT inayoongoza Ligi Kuu na pointi 27, baada ya kucheza mechi 15, inashuka kwenye Uwanja wa Isamuhyo ikitoka kushinda bao 1-0, dhidi ya Mashujaa, huku kwa upande wa Coastal Union ikitoka kuifunga pia maafande wa Tanzania Prisons mabao 4-1.
Mechi hiyo itakayopigwa saa 10:00 jioni, ni ya nane kwa Coastal Union kucheza ugenini kwa msimu huu, ambapo kati ya saba zilizopita, kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’, kimeshinda mmoja ambayo ni ushindi wa 4-1, dhidi ya maafande wa Prisons.
Mbali na hilo, ila mabao manne iliyofunga Coastal Union katika mechi dhidi ya Prisons, yalikuwa ni ya kwanza kufunga kwa kikosi hicho kikiwa ugenini, kwani kabla ya hapo kilikuwa hakijawahi kufunga zaidi ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa tu.
Kwa upande wa JKT, hii ni mechi ya 16, msimu huu, japo ni ya tisa kucheza nyumbani, ikishinda tatu, ikitoka sare tatu na kuchapwa miwili ambayo ni mabao 2-1, dhidi ya Simba, Novemba 8, 2025, kisha 1-0, mbele ya Dodoma Jiji, Januari 30, 2026.
Mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Septemba 22, 2025, JKT ilishinda mabao 2-1, yaliyofungwa na Salehe Karabaka na Mohamed Bakari, huku la Coastal Union likifungwa na Athumani Masumbuko ‘Makambo’.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, alisema anatarajia mechi ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu hasa raundi hii ya pili, huku kwa upande wa Mohamed Muya wa Coastal Union akijivunia utayari wa nyota wa kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wenyeji Mtibwa Sugar itaikaribisha Mashujaa kuanzia saa 12:30 jioni, huku kikosi hicho cha maafande kikiwa na mwenendo usioridhisha hadi sasa, hali iliyochangia pia kumwondoa Kocha Mkuu, Salum Mayanga.
Mtibwa inayonolewa na Mkenya Yusuf Chippo, akishirikiana na Awadh Juma ‘Maniche’, tangu alipojiunga na timu hiyo rasmi, Novemba 17, 2025, hajawahi kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara, akishinda nne na kutoka sare nne kati ya nane alizoiongoza.
Chippo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, alijiunga na kikosi hicho Novemba 17, 2025, baada ya kuachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu, Agosti 21, 2025.
Kwa upande wa Mashujaa, haijaonja ladha ya ushindi katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu Bara baada ya kuchapwa nne na kutoka sare tatu tu, huku mara ya mwisho kushinda iliifunga Mbeya City bao 1-0, ikicheza nyumbani, Novemba 22, 2025.
Hata hivyo, mechi ya kwanza kati ya timu hizo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, kikosi hicho cha maafande wa Mashujaa kiliifunga Mtibwa Sugar bao 1-0, Septemba 21, 2025, lililofungwa na Idrisa Stambuli dakika ya 32.