UMOJA wa Ulaya (EU) umeonesha nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika mnyororo wa thamani wa madini. Mnyonyoro huo ni pamoja na ujenzi wa uwezo kwa wataalamu wa madini, mafunzo ya ufundi stadi, teknolojia za kisasa na utunzaji wa data na takwimu.
Hayo yameelezwa katika majadiliano baina ya Wizara ya Madini na wadau wa kimataifa katika Kongamano la Madini la Indaba 2026 linaloendelea jijini Cape Town nchini Afrika Kusini. EU ilieleza Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na Programu ya PanAfGeo ambayo ni mpango wa EU unaolenga kuimarisha uwezo wa taasisi za utafiti wa jiolojia Afrika, ikiwamo Tanzania. SOMA: Burkina Faso yaja Tanzania kujifunza Sekta ya Madini
Aidha, EU imeahidi kushirikiana na serikali kutafuta masoko ya madini Ulaya na kuwatengenezea mazingira wezeshi wawekezaji, waweze kutekeleza shughuli za uongezaji thamani madini ndani ya nchi. Mavunde alisema serikali itaendelea kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa haraka wa miradi ya madini na kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Amesema Tanzania na Afrika wapo tayari kushirikiana na wawekezaji na sekta binafsi kwa ujumla kuvuna rasilimali za madini kwa manufaa ya pamoja. Mavunde amesema Afrika inalenga kubadilika kutoka kusafirisha madini ghafi kwenda katika uongezaji thamani ndani ya nchi zake.
Amesema mtazamo wa Afrika kuhusu usimamizi wa rasilimali haulengi kuwatenga wawekezaji, kuleta kutokutabirika kwa sera au kutafuta faida za muda mfupi. Mavunde amesema mtazamo huo unalenga kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji, uwazi na kwa kuzingatia sheria ili ziwe chachu ya maendeleo ya muda mrefu kwa nchi husika na wananchi wake. Ametoa mfano wa Tanzania kuwa msimamo huo si kikwazo cha uwekezaji, bali ni msingi wa kujenga ushirikiano endelevu.
Mavunde amesema usimamizi wa rasilimali unahusisha kuheshimu mikataba na mifumo ya kisheria, kutoa uhakika na utabirikaji wa sera kwa wawekezaji, kuhakikisha thamani ya haki kwa mataifa ya Afrika na jamii zinazozunguka miradi ya madini na kuhimiza uongezaji thamani na uwekezaji wa muda mrefu katika mazingira yenye taasisi imara, sera thabiti na uhalali wa kijamii.

Amesema Dira ya Madini ya Afrika, ajenda ya maendeleo ya Tanzania na kaulimbiu ya Indaba zinakutana kwenye msingi kwamba ushirikiano ni daraja kati ya dira na mitaji. Mavunde amesema madini yanahitaji mitaji, ushirikiano baina ya serikali na wawekezaji na mipango ya miundombinu. Amesema Tanzania inajenga ushirikiano katika msingi wa kuaminiana, uwazi na mgawanyo sawia wa manufaa kwa kila upande.
Katika kikao kilichofanyika baina ya Mavunde na Kampuni ya Madini ya Barrick, kampuni hiyo imeahidi kushirikiana na Tanzania kuhaulisha ujuzi kwa wafanyakazi wa wizara kupitia mafunzo ya vitendo. Pia, alieleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora katika sekta ya madini inalenga kuwezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kwa tija katika uchumi wa madini.
Ujumbe wa Kampuni ya Madini ya Sotta inayomiliki mradi wa uchimbaji wa dhahabu wa Nyanzaga wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza umeishukuru serikali kwa ushirikiano kuendeleza mradi huo. Kampuni hiyo imeomba majadiliano zaidi ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa wazabuni wazawa kwa ajili ya kutoa huduma kwenye mgodi huo unaotarajiwa kuanza uzalishaji katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.