TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imeendelea na vikao vyake leo Februari 13, 2026 kwa kukutana na Wakuu wa Majeshi Wastaafu, Davis Mwamunyange na George Waitara, kwa nyakati tofauti.
Mikutano hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Tanganyika uliopo katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume kukusanya taarifa, maoni na ushauri kutoka kwa viongozi wakuu wa zamani kuhusu matukio hayo. SOMA: Tume yakutana na Makamu wa Rais Mstaafu

Katika kikao na Jenerali Mwamunyange, Tume ilijadili kwa kina chanzo cha matukio ya uvunjifu wa amani, athari zake kwa wananchi, mali na miundombinu, pamoja na mapendekezo ya namna ya kuzuia matukio kama hayo yasijirudie.
Kwa upande wa Jenerali Waitara, mjadala ulijikita katika tathmini ya athari za matukio hayo na ushauri wa hatua za kijamii na kisheria zinazoweza kuchukuliwa kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa. Tume inaendelea kukutana na makundi mbalimbali, ikiwemo waathirika wa matukio hayo katika mikoa tofauti nchini, kwa lengo la kukusanya ushahidi na taarifa zitakazosaidia kuandaa ripoti ya kina.