Wakazi wa Mtaa wa Mlimani, Kata ya Mkundi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, wamekamilisha ujenzi wa karavati kwa kumwaga zege upande mmoja wa kolongo linalotenganisha Mtaa wa Msimamo na Mtaa wa Mlimani, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano hasa wakati wa mvua.
Mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni tatu umefadhiliwa na wananchi wenyewe kupitia michango yao ya hiari, wakilenga kupunguza adha ya kukatika kwa mawasiliano kati ya mitaa hiyo miwili.
Baadhi ya wananchi wameiambia Channel Ten kuwa kwa zaidi ya miaka kumi wamekuwa wakichonga na kutengeneza barabara kwa nguvu zao, hivyo walipoona changamoto ya kolongo hilo kuleta kero, waliamua kuunganisha nguvu na kuchangia kidogo kidogo hadi kufanikisha ujenzi huo, licha ya ugumu wa hali ya uchumi.
Hata hivyo, wananchi hao wameiomba serikali kuwajengea daraja la kudumu katika eneo hilo, wakieleza kuwa wakati wa mvua watoto hushindwa kwenda shule na huduma za usafiri husimama, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi.
Kwa upande wake, Mjumbe na Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani, Haji Mrisho Mbonde, amesema serikali ya mtaa kwa kushirikiana na mabalozi walikubaliana kuchangisha fedha ili kutatua changamoto zilizopo, huku wakiendelea kutafuta wadau na kusubiri msaada zaidi kutoka ngazi za juu.
(Feed generated with FetchRSS)