1. Vipindi vya Redio ya Umoja wa Mataifa vilitoa tafsiri sahihi ya wapigania uhuru
Leo ni siku ya redio duniani ambayo msingi wake unatokana na kuanzishwa kwa redio ya Umoja wa Mataifa tarehe 13 Februari mwaka 1946 jijini New York, Marekani. Kwa mantiki hiyo ikiwa mwaka huu redio hiyo ya Umoja wa Mataifa inatimiza miaka 80 tumeangazia mchango wa vipingi vyake vilivyokuwa vinarushwa na redio zingine ikiwemo iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) nchini Tanzania wakati huo
Edda Sanga, Mtangazaji nguli nchini Tanzania ambaye alikuwa Msimamizi wa Vipindi kwa iliyokuwa Redio Tanzania sasa Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC.
Sauti hiyo ni ya Edda Sanga, mtangazaji nguli nchini Tanzania ambaye alikuwa Msimamizi wa Vipindi kwa iliyokuwa Redio Tanzania sasa Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC, akizungumza nami kuhusu mchango wa kipindi cha Mwangaza wa Umoja wa Mataifa kilichokuwa kinaandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na kurushwa na kituo hicho.
“Lakini pia wasikilizaji kwa ujumla wao kutokana na kipindi hiki cha mwangaza, kwa kweli walipata manufaa mengi sana. Walipata maarifa mapya, lakini pia walipata habari mbalimbali zilizohusu mizozo mbalimbali ambayo ilikuwa inatokea katika baadhi ya nchi nyingine. Zikiwa ni hawa majirani zetu, lakini pia walipata habari kutokana na namna ambavyo mijadala ilikuwa inaendelea katika Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, kwa kipindi hicho na kwa sababu pia redio zilikuwa chache, sio nyingi kama zilivyo hii leo, tumaini kubwa lilikuwa kwa mwangaza ambao ulitoka mara moja kwa wiki kwa muda wa robo saa, na walikuwa wakingojea kipindi hiki kwa hamu. “
Miaka ya 70, 80 na 90 ilishuhudia Tanzania ikiwa kituo cha wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika. Nikamuuliza Bi. Edda Sanga mchango wa kipindi cha Mwangaza wa Umoja wa Mataifa katika harakati hizo.
“Na wakati ule ilikuwa pia masuala ya wapigania uhuru kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika ambao pia tulikuwa nao. Na hawa basi habari zao zilikuwa zinatangazwa sana na kipindi chetu hiki cha mwangaza zikitoa hata kupinga yale ambayo wenzetu walikuwa wanaita kwamba hawa ni magaidi. Lakini sisi tulijua kwamba hawa ni wapigania uhuru. Sasa pia tuliona kwamba katika kipindi hiki kulikuwa na fursa za sauti za wananchi uwepo na pia fursa ya kuelezea nini ambacho wanakiona kizuri kuhusu kipindi hicho, kitu ambacho ni kizuri wakati wote.”
Na zaidi ya yote.
“Na hatimaye pia niseme kilichonivutia pia ni kujenga matumaini na matamanio kwa walio wengi. Katika kupitia kipindi hiki ambayo imesaidia sana kujikita na kuonesha mafanikio mbalimbali na suluhu ambazo zilikuwa zinapatikana hasa katika mizozo na migongano na mambo mengi sana ambayo yalikuwa yanatokea wakati huu.”
2. Redio Okapi iliokoa maisha yangu: Mkimbizi Bahati Yohane
Katika maeneo ya migogoro,duniani redio huwa nguzo ya utulivu na wakati mwingine daraja la kuokoa maisha. Na ndivyo ilivyokuwa kwa mkimbizi Bahati Yohane kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwani kwake, redio haikuwa tu combo cha habari ilikuwa dira ya kuokoa maisha yake.
Mkimbizi Bahati Yohane kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambaye anaishi katika makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda.
Akizungumza kutoka kambi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda, mkimbizi huyo amekumbusha namna matangazo ya redio Okapi ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC ujulikanao kama MONUSCO yalivyomsaidia kufanya uamuzi mgumu wa kukimbia vita nchini mwaka mwaka 2008 na kwenda nchi jirani ya Uganda.
Katika kuadhimisha siku hii ya Redio Duniani Bahati Yohane amesema “Siku ya leo inanikumbusha nyumbani kwetu. Mara nyingi tulikuwa tunasikiliza redio. Wakati usalama ulikuwa mdogo, redio ilitangaza na kutuambia sehemu fulani si salama na hivyo tunakimbia,” alisema.
Kambi ya wakimbizi ya Kyangwale nchini Uganda.
Tangazo lililobadili maisha yake
Kwa mujibu wa simulizi yake, mwaka 2008 hali ya usalama ilizidi kuwa mbaya katika eneo lao mashariki mwa DRC. Ilikuwa kupitia redio Okapi ndipo walipopata taarifa muhimu kuhusu maeneo ya kujinusuru.
“Nakumbuka walitangaza wakasema hali imekuwa mbaya sana. Wakasema wale walioko mpakani mwa Uganda waingie Uganda. Hapo hapo nikashika familia yangu tukaanza safari. Ilikuwa vita,” ameeleza kwa msisitizo.
Yohane anasema bila taarifa hizo za redio, huenda uamuzi wa kuondoka usingefanyika kwa wakati, na madhara yangekuwa makubwa zaidi.
Mwandishi wa habari anafanya kazi katika ofisi iliyoharibiwa huko Gaza
3. Wito wa kuimarisha matangazo ya lugha mbalimbali
Sasa akiwa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kyangwali, mkimbizi huyo anasisitiza umuhimu wa kuimarisha matangazo ya redio kwa lugha mbalimbali ili kuwafikia wakimbizi wote, hasa wale wasiozungumza Kiswahili au lugha za wenyeji.
Kwa mujibu wa Yohane kambi ya Kyangwali ina wakimbizi kutoka mataifa na makabila tofauti, wenye lugha mbalimbali hali inayoweza kuwa kikwazo kwa upatikanaji wa taarifa muhimu.
“Kyangwali kuna watu tofauti, makabila tofauti na lugha ni nyingi. Kuna wale ambao hawajui Kiswahili. Kama kungekuwa na redio hapa yenye lugha mbalimbali, mawasiliano yangekuwa rahisi sana kwa wakimbizi,” amesisitiza.
Kituo cha redio cha Zaman FM Radio katika Gaza hivi karibuni kimerudi hewani kwa kutumia uwezo mdogo wa kiufundi, kikifanya kazi kutoka makao yake makuu yaliyoharibiwa.
Redio bado ni muhimu
Katika dunia ya sasa ya mitandao ya kijamii na simu janja, ushuhuda huu wa Bahati Yohane unaonesha kuwa redio bado ni chombo muhimu cha mawasiliano ya dharura, hasa katika mazingira ya migogoro na uhamishaji wa watu.
Kwa wakimbizi wengi, redio si tu chanzo cha habari ni sauti ya tahadhari, mwongozo wa usalama na wakati mwingine, tumaini la kuanza maisha mapya.
Kabla ya vita vya sasa kuanza katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina lilalokaliwa kimabavu na Israel, Redio ilikuwa chombo muhimu kwa umma na kwa hakika umuhimu wake haujakoma isipokuwa huduma ya matangazo ya redio ndio iliyokuwa imekoma kutokana na vituo vya redio kusambaratishwa kwa makombora, lakini sasa juhudi zinafanyika kuirejesha huduma hiyo muhimu. Anold Kayanda na taarifa zaidi.
Baadhi ya vituo vya redio vya ndani ya Ukanda wa Gaza vimeanza tena kurusha matangazo baada ya kusimamishwa kwa karibu miaka miwili kutokana na vita, hatua inayodhihirisha juhudi za taratibu za kufufua mazingira ya vyombo vya habari katika eneo hilo ambalo limekumbwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu na taasisi za kiraia.
Miongoni mwa vituo hivyo ni Zaman FM, hivi karibuni kimerudi hewani kikitumia uwezo mdogo wa kiufundi ambapo wafanyakazi wanaendelea kufanya kazi wakiwa ndani ya magofu huku wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa na rasilimali muhimu.
Redio zinazorusha matangazo kutoka Gaza bado ni muhimu sana wakati majanga ya kibinadamu yakiendelea, mathalani kukatika kwa umeme.
Mwanahabari Rami Al-Sharfi, ni mkurugenzi wa redio katika kituo cha redio cha ZMN 90.60 FM cha Gaza.
Rami Al-Sharafi, Mkurugenzi wa Zaman FM na mtangazaji wa vipindi, anasema vituo 23 vya redio vya ndani vilikuwa vinafanya kazi Gaza kabla ya tarehe 7 Oktoba 2023, lakini vyote vililazimika kusitisha matangazo baada ya kuharibiwa wakati wa vita, ila sasa,
“Leo, Zaman FM imeanza tena kurusha matangazo, na kwa sasa sisi ndio kituo pekee cha redio kinachorusha mawimbi ya FM kutoka ndani ya Ukanda wa Gaza baada ya uharibifu huu mkubwa. Tunatumaini vituo vingine vya redio vya ndani vitarejea kufanya kazi, ili kuwe na ushindani wa kitaaluma katika kuhudumia umma wa Wapalestina katika Gaza.”
Anaendelea akisema,
“Gaza inahitaji kwa dharura vituo vya redio vya kitaaluma vinavyoweza kurusha ujumbe wa uhamasishaji kwa umma na matangazo ya mwongozo, hasa wakati wa kuenea kwa magonjwa na kuporomoka kwa mfumo wa elimu. Tunahitaji haraka kuwapatia wakazi taarifa na taarifa mpya za ushauri, hasa magonjwa ya mlipuko yanapoenea na baadhi ya huduma zikiendelea kusitishwa au kurejea taratibu, ili wananchi wajue wapi pa kupata huduma muhimu mara vita vitakapomalizika.”
Kuanza tena kwa matangazo ya redio kunakuja wakati miundombinu ya vyombo vya habari Gaza ikiendelea kukabiliwa na changamoto kubwa, huku kukiwa na wito wa ndani na wa kimataifa wa kuunga mkono vyombo vya habari kama sehemu ya juhudi pana za uokoaji na ujenzi upya wa eneo hilo la mashariki ya kati.