Algeria jana Ijumaa ilianza kusafisha baadhi ya maeneo ya majaribio ya silaha za nyuklia yaliyofanywa na Ufaransa katika jangwa la nchi hiyo katika kipindi cha ukoloni, miaka ya 1960.
Shirika la Habari la Algeria limeripoti kwamba nchi hiyo imeanza operesheni ya kwanza ya kusafisha maeneo ya majaribio ya silaha za nyuklia ya Ufaransa huko “Beriel”, katika eneo la “Taourirt Tan Afella” katika jimbo la Tamanrasset (kusini), baada ya miongo kadhaa ya utafiti na mipango, juhudi na kwa uwezo wa kitaifa.
Operesheni hiyo imetangazwa sanjari na maadhimisho ya miaka 66 ya majaribio ya silaha za nyuklia ya Ufaransa, ambayo yanaendelea kuchafua maeneo makubwa ya Algeria na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.
Hatua ya Algeria ya kusafisha maeneo ya majaribio ya nyuklia inakuja baada ya Algiers kuitaka Ufaransa mara kadhaa ikabidhi ramani za maeneo zilikozikwa taka za nyuklia.
Nyaraka zinaonyesha kwamba eneo la “In Eker” lilishuhudia mlipuko wa chini ya ardhi wenye nguvu ya tani 150,000 za TNT, ambao ulisababisha uvujaji wa gesi zenye mionzi zilizosababisha uharibifu kamili wa mfumo ikolojia.
Nyaraka hizo zinaonesha kuwa eneo hilo bado linateseka – hadi leo – kutokana na uzalishaji wa mada hatari kama vile “Cesium-137” na “Plutonium”.
Kila mwaka tarehe 13 Februari, Algeria hukumbuka jaribio la kwanza la silaha za nyuklia lililofanywa na Ufaransa katika jangwa la Reggane katika jimbo la Adrar kusini mwa nchi, mwaka wa 1960. Nguvu ya mlipuko huo ilikuwa mara 5 zaidi ya bomu lililotumiwa na Marekani huko Hiroshima nchini Japani, na operesheni hiyo ilipewa jina la “Blue Jerboa”.

Algeria inaona majaribio hayo kuwa yametimiza vipengele vyote vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa na utawala wa kikoloni wa Ufaransa dhidi ya Waalgeria.