Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa sanaa kwa ujumla, huwa kunatokea watu ambao hupata umaarufu mkubwa japo hawajafanya makubwa katika shughuli za sanaa. Na vivyo hivyo kuna maelfu ya wasanii huwa hawabahatiki hata kutajwa japo unaweza kukuta wana historia kubwa katika shughuli za sanaa. Hakika usemi wa hawavumi lakini wamo una maana kubwa.

Wiki iliyopita nilishiriki mazishi ya ndugu yangu na rafiki yangu ambaye waliomfahamu kwa miaka ya karibuni walimjua kama Mhadhiri wa Idara ya Famasia, katika Chuo Kikuu cha ST John Dodoma. Huyu ni Joseph Anselm Mkwawa. Joseph alizaliwa mwaka 1956 pale Iringa. 

Hakukuwa na dalili zozote za uanamuziki katika miaka yake ya awali, mpaka alipoingia sekondari.  Kama ilivyokuwa kawaida ya shule nyingi za sekondari katika miaka ya 1960 na 1970, shule kuwa na bendi lilikuwa jambo si geni na Joseph na wenzie katika shule ya sekondari ya Old Moshi walikuwa na bendi yao iliyokuwa maarufu kwa kujiita ufupisho wa jina la shule yao MOSESCO Jazz Band. Joseph alikuwa mpiga gitaa la bezi.  

Kwa walikuwa wakiifahamu historia ya familia ya Joseph haikuwa ajabu yeye kuwa mwanamuziki. Babu yake, Mzee Pangaras Mkwawa, alikuwa maarufu kwa upigaji wa  gombo la Kisangu. Watoto waliokulia mitaa ya Mshindo miaka ya 60 walimfahamu sana mzee huyu kwani pia alikuwa na gari la punda alilokuwa akipita nalo katikati ya mji akienda kwenye shughuli zake. 

Mzee Pangras alikuwa mpigaji mzuri sana wa gombo, mwaka 1951 aliwahi kurekodiwa na mtafiti wa muziki aliyeiywa Hugh Tracey hivyo nyimbo zake zinapatikana mpaka leo. 
Wakati wa kurekodi nyimbo hizo, mtoto wa Mzee Pangras, Anselm, ambaye ndie baba yake Joseph alishiriki kwa kumsindikiza baba yake kwa kupiga vijiti. Muziki katika ukoo wa Mkwawa sio kitu kipya kwani hata baba yake Mzee Pangras,  Chifu Mkwawa mwenyewe alikuwa fundi wa kupiga gombo.

Gombo lake lililochukuliwa na askari wa Kijerumani baada ya Chifu Mkwawa  kujiua na bado liko  katika makumbusho ya Humboldt kule Berlin Ujerumani. Nilianza kumuona Joseph akipiga gitaa mwaka 1974.

Bendi yao ilikuwa nzuri sana ikiwa na wanamuziki wanafunzi kama akina Tamba, Peregreen, Kufakunoga na wengine wengi. Ilikuwa ni katika bendi hii nilipofundishwa namna ya kupiga mtindo wa kent aliokuwa akiutumia Franco. 

Wimbo wa Djemelasi ulikuwa ndio unatamba na hapo nikafundishwa namna ya kupiga solo lile lililopigwa na Mose Fan Fan. Kitu kingine nilichokikuta katika bendi ya kina Joseph ni ile staili mpya ya kupiga gitaa la ridhim ambayo iliibuka na upiga ridhim wa kina Vata Mombasa kwenye mtindo wao wa Kavacha.

Upigaji huo ulikuwa unatumia ufungaji wa nyuzi ulioitwa double string. Wakati huo Moshi kulikuwa na bendi kadhaa, ikiwemo Zaire Success, Bana Afrika Kituli, na bendi ya Chuo Cha Polisi maarufu PTS na Moshi Technical School nao walikuwa na bendi yao. Ukumbi wa YMCA ulikuwa haukosi shughuli ya muziki siku za mwisho wa wiki. Baada ya kumariza shule Joseph alienda JKT na ilikuwa ni nyakati za mgogoro wa nchi yetu na Uganda, hivyo alikuwa mmoja wa vijana waliolazimika kwenda  mstari wa mbele kutetea nchi.

Mwaka 1978, mtafiti mmoja wa muziki, John Low, alikuwa anazunguka Afrika ya Mashariki kutafuta wapiga magitaa baridi. Alienda Kongo akakutana na Losta Abelo nakumrekodi, akakutana na wapiga magitaa wengine maarufu kama Losta Abelo, Kayembe Yirung,  Soki Nambi na Chola Piana  akapita Zambia na hatimae  Tanzania na kwenda Iringa ambako alikuwa akimtafuta Francis Kitime. Hakumkuta kwani alikuwa amesafiri kwenda Dar es Salaam. Alimfuata Dar es Salaam na kumkuta akiwa kwa dada yake ambaye pia ni mama mkubwa wa Joseph Mkwawa.

Baada ya kujieleza kuhusu utafiti wake, Francis aliweza kurekodi nyimbo nane. Joseph nae ambaye wakati huo alikuwa ameanza kufundisha Ufamasia katika chuo cha Muhimbili nae alikuwepo na akarekodi nyimbo zake nne. 

Ilichukua miaka 16 ndipo walipopata habari kuwa nyimbo walizorekodi zilisambazwa kama CD huko Ulaya. Mwaka 1996 waliweza kupata kifuta jasho kutoka kwa msambazaji.

Miezi michache iliyopiya kampuni moja ya usambazaji nchini Marekani ilianza kuonyesha nia ya kuzisambaza upya nyimbo hizo lakini zikiwa kwenye santuri. Bahati mbaya kabla hili halijatimia Joseph ameaga dunia, Francis Kitime alikwisha aga dunia mwezi wa Agosti  mwaka 2015. 

Joseph hakika hakujulikana kama mwanamuziki lakini alifanya mengiu katika muziki kwenye miaka ya 1980 alienda kusoma Urusi na huko akiwa na wenzie walitengeneza bendi yao iliyokuwa ikiwatumbuiza wenzao. Bahati mbaya sana mwaka 2017 alipata stroke hivyo hakuweza tena kupiga gitaa mpaka mauti yalipomkuta Mungu amlaze pema Joseph Anselm Mkwawa.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *