Chama cha Jamaat-e-Islami, chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini Bangladesh, kimehoji matokeo ya uchaguzi uliofanyika nchini humo majuzi, ambapo kimeshika nafasi ya pili kwa kupata viti 74 baada ya Chama cha Kizalendo cha Bangladesh, ambacho kumeshinda viti 212 kati ya 300 vya Bunge.

Baada ya kiongozi wa Jamaat-e-Islami, Shafiqur Rahman kukubali kushindwa na kuahidi kufuata “siasa chanya,” chama chake kilitangaza jana Ijumaa kwamba kina “maswali mazito kuhusu usahihi wa matokeo ya uchaguzi wa Bunge.”

Kundi hilo la Kiislamu limesema katika taarifa yake kwamba: “Haturidhiki na mchakato unaozunguka matokeo ya uchaguzi,” likilaani kuwepo “utata au udanganyifu uliokaririwa katika kutangazwa matokeo ya awali,” suala ambalo limesema “linazua maswali mazito kuhusu uadilifu wa mchakato huo.”

Kwa upande wake, Chama cha Kizalendo cha Bangladesh (Bangladesh Nationalist Party), kimetangaza kuwa kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo, ukiwa wa kwanza kufanyika nchini humo tangu baada ya uasi wa mwaka 2024 uliomng’oa madarakani Waziri Mkuu, Sheikh Hasina.

Chama cha BNP kinaongozwa na Tarique Rahman, mgombea wake wa uwaziri mkuu, ambaye alirejea Bangladesh mwezi Desemba mwaka jana baada ya kuishi uhamishoni mjini London kwa kipindi cha miaka 17

Tarique Rahman mwenye umri wa miaka 60 ni mtoto wa waziri mkuu wa zamani wa Bangladesh, Khaleda Zia, ambaye alifariki dunia Desemba mwaka jana.

Muungano wa vyama vya Kiislamu, Jamaat-e-Islami, utawakilisha kambi ya upinzanii katika bunge jipya baada ya kupata idadi isiyo ya kawaida ya viti, ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi uliopita, ambapo hakikupata zaidi viti 18.

Chama cha Kitaifa cha Wananchi, kilichoanzishwa na vijana wa harakati za wanafunzi, au Gen Z kimeshika nafasi ya tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *