Dar es Salaam. 2006 ndio mwaka ambao Kamati ya Miss Tanzania. Chini ya ‘Anko’ Hashim Lundenga (RIP), ilituletea mastaa wakubwa wa kike nchini. Ambao hadi leo bado wana ustaa wao. Wanakimbiza mjini sana.

Natamani ‘pati’ kubwa ifanyike. Kutimiza miaka 20 ya Miss Tz bora zaidi, iliyozalisha warembo maarufu sana nchini. Ndiyo, hapa panahitajika akili mtambuka zaidi kufanya hili litokee.

Kuna Madam Wema. Pale kuna Jokate na bibie Irene Uwoya yupo kule. Kuna Lissa Jensen katulia, usisahau na pale katikati yupo Anti Ezekiel. Hawa wana dunia yao ya majina makubwa ya kike Bongo

Mwigizaji Irene Uwoya

Hii imekaa kikuda sana. Kama bado ‘laifu’ lako la kuungaunga usisogeze pua yako kwa hizi pisi. Hawa ndo dadaz waliofanya Jiji la Dar es Salaam, liwe la joto kwa miaka 10 mfululizo bila kukauka. Usipime hata nusu majina haya.

Mambo ya kuamsha dude na kutengeneza taharuki siyo shida zao. Wanaweza kulifanya taifa liwaongeleee kwa wiki au mwezi mzima. Wanatengeneza stori kuliko wanasiasa wakiamua na wanamichezo.

Unachopaswa kujua, kwa kiasi kikubwa dadaz hawa wameikuza sanaa yote ya filamu. Siyo filamu tu bali na waigizaji wengi nchini wamefunguliwa njia na wao. Yes, wanastahili kupewa sifa kubwa kwenye hili hawa dadaz.

Wameshiriki kuukuza muziki na wanamuziki. Bongo Fleva kwa ujumla na wana Bongo Fleva, ni sahihi sana kuwatazama dada hao kama sehemu ya ujenzi wa ‘gemu’ lao. Kimsingi walikuwa chombeza sahihi ya sanaa.

Safari ya Diamond Platinumz. Ni wazi kwamba haiwezi kusimuliwa bila jina la Wema Sepetu. Madam huyu kwa kiwango cha juu sana alishiriki kumtengeneza Diamond huyu wa sasa. Ukatae ndo hivyo ukubali ndo hivyo. 

Lugha ya Kiingereza ambayo leo inamsaidia Mondi kwenye mishe zake. Kuna jasho la Wema kwa kiwango kikubwa. Alifanya kazi ya kumtengeneza Mondi ili aweze walau kupiga stori na Davido na akaeleweka. Lugha laini ya Wema.

Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006

Hili alishakiri Mondi mwenyewe katika mahojiano yake kadha wa kadha. Kwamba Wema Sepetu ndiye mwalimu wake wa ngeli. Achana na Zari The Boss Lady. ‘Aliyesimenti’ lugha hiyo kwenye kinywa cha Mondi, naye yumo.

Kuna Whozu mwanamuziki, na Whozu supastaa baada ya Wema kujimilikisha mbavu zake. Hapa anaweza kuwa mwanamuziki mzuri lakini uwepo wa Wema uliongeza thamani yako. Hili lilimsaidia hata Chaz Baba wa Twanga Pepeta.

Chaz Baba aliwahi kumiliki penzi la Wema. Jina lake likawa kubwa katikati ya wanamuziki wenzake wa Twanga. Hata mahudhurio ya mashabiki kwa shoo za Twanga, uliongezeka. Waliokuwepo kwa wakati ule wanakumbuka jinsi Mango Garden ilivyokuwa.

Kwa sababu ya ‘drama’ za Wema na Chaz Baba. Twanga Pepeta ikawa inakimbiza kinoma mbele ya bendi zingine. Na Chaz Baba pia akawa staa mkubwa mbele ya wasanii wa dansi. Akazipamba kurasa za magazeti ya udaku ‘dei tu dei’.

Mwigizaji Aunt Ezekiel ambaye ni mke wa msanii wa Bongo Fleva Kusah

Jojo naye jina na sura yake kwa kiwango kikubwa ilisaidia sana kuikuza sanaa ya muziki. Uwepo wake kando ya mbavu ya Alikiba, huwezi kumuweka kando kama mmoja wa pisi zilizolinogesha gemu la muziki. 

Kulikuwa na muziki mzuri sana wa Alikiba. Na kulikiwa na penzi na uhusiano mzuri wa Alikiba na Jokate. Labda kama hujui ubora na thamani ya Jokate, unaweza kuuliza alisaidia nini kwa ukuaji wa gemu?

Ndivyo ilivyo kwa Anti Ezekiel na Mose Iyobo. Nani aliamini kama pisi kali Anti angejizima data na kujiweka jumla jumla kwa dansa wa msanii wa Bongo Fleva? Yes, na mtoto akamzalia na kuifanya gemu ya madansa inogeshwe. 

Kuna Irene Uwoya na Dogo Janja. Ndiyo pamoja na uwepo wake kabla ya kuwa penzini na Uwoya, lakini ndoa yao (hata kama feki), ilikuza jina la Dogo Janjaro. Na hata muziki wake ulibadilika na kuwa mkubwa zaidi. 

Miss Tanzania 2006 ni mastaa walitengeneza mastaa kupitia majina yao. Waheshimiwe kwa kujenga maisha ya wengine kaa kutumia majina yao. Kwanini basi kisifanyike kitu mwaka huu 2026, ikiwa imepita miaka 20? 

Kama siyo basi kitu kifanywe na wale ambao. Maisha hao kwa ujumla yalibadilika kwa kudili na warembo hawa. Hata Kanumba jina lake lilipaa zaidi baada ya kugundulika kuwa anatoka na Wema. Waliokuwepo hawawezi kusahau. 

Jack Wolper anaweza kusapoti haya kama siyo mmoja wa Miss Tz 2006. Na yeye jina lake kwa kiasi kikubwa lilichangia sana kukuza sanaa na wasanii wake akiwepo Konde Boy.  Wanaatahili kupewa sifa kubwa kwa hili.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *