Dar es Salaam. Ni vigumu kuzungumzia mafanikio ya staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz (36) katika anga la muziki kimataifa bila kulihusisha jina la Davido (33) kutokea Nigeria ambaye wikiendi iliyopita alifanya show nchini.
Hata hivyo, mbali na ushirikiano wa kazi na nguvu yao ya ushawishi katika muziki Afrika. Idadi ya wafuasi (followers) walionao katika mtandao wa Instagram ni eneo lingine linalopima ubavu wa chapa zao.
Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, alitoka rasmi kimuziki kupitia wimbo wake, Kamwambie (2009) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza iliyoachiwa mwaka uliofuatia.
Alishinda tuzo yake ya kwanza katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010. Na tangu wakati huo aliendelea kufanya vizuri na hadi sasa akiwa ameshinda tuzo zaidi ya 20 za TMA.
Baada ya kutoa albamu mbili, Diamond alianza harakati za kutaka kusikika kimataifa, na hapo ndipo jina la Davido lilianza kuchukua nafasi katika safari ya muziki wake.
Davido, mwanzilishi wa Davido Music Worldwide (DMW), yeye alipata umaarufu alipoachia wimbo wake, Dami Duro (2011). Ila kwa hapa Bongo alivuma zaidi kupitia ngoma yake, Aye (2014).
Mwaka 2013, Davido alikuja kufanya show hapa nchini na ndipo Sallam SK ambaye aliyehusika kumleta, akamkutanisha na Diamond na ndipo ikarekodiwa ngoma, My Number Remix (2014).
Baadaye walienda Nigeria kwa ajili ya kushuti video, na remix hiyo ilipotoka ikafanya vizuri, na pia ndio ukawa mwanzo wa Sallam SK kuwa meneja wa Diamond, jukumu ambalo bado yupo nalo hadi wakati huu.
Kuanzia hapo jina la Diamond likaanza kuzungumzwa kwa ukubwa Afrika akiwania tuzo kubwa kama MTV MAMAs kwa mara ya kwanza, kisha mwaka uliofuatia akashinda tuzo mbili za MTV EMAs.
Mafanikio hayo yalipelekea ushawishi wa Diamond kuongezeka kwa asilimia kubwa, na hadi kufikia Desemba 2015. Akawa ndiye mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram barani Afrika akimpiku Davido.
Ikumbukwe mastaa hao walipishana miezi mitatu kujiunga katika mtandao huo ulioanzishwa Oktoba 2010 na Kevin Systrom na Mike Krieger, kisha kuja kununuliwa na kampuni ya Meta, zamani Facebook.
Sasa hiyo Desemba 2015, Diamond aliyejiunga na Instagram mnamo Julai 2012, alifikisha wafuasi milioni 1.5, akimpiku Davido aliyekuwa na milioni 1.4 tangu alipojiunga Machi 2012.
Baada ya Diamond na Davido, wanamuziki waliofuatia wakati huo ni Wizkid, Don Jazzy, na Vanessa Mdee, mkali wa Bongofleva aliyetoka na kibao chake, Closer (2013) chini ya Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group.
Hata hivyo, kufikia Septemba 2016, Davido akarejea namba moja Instagram akifikisha wafuasi milioni 2.9, huku Diamond akishuka hadi namba mbili akiwa na wafuasi milioni 2.5.
Wakati huo wanamuziki waliowafuatia ni Don Jazzy, Tiwa Savage, Vanessa Mdee, Alikiba, na Yemi Alade, kipaji kilichoibuliwa na Peak Talent Show 2009, kisha kuja kuvuma na ngoma yake, Johnny (2014).
Kwa sasa Davido anaendelea kuwa mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni 31.4, huku Diamond akiwa na milioni 18.9, na kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya Tiwa Savage kutokea Nigeria.
Ni wazi kwa namna mambo yanavyoenda, kuna uwezekano mdogo sana kwa Diamond kuja kumpiku tena Davido na kuwa namba moja Afrika kwa kuwa na wafuasi wengi Instagram upande wa wanamuziki kama alivyofanya 2015.
Tayari Davido amemuacha Diamond kwa wafuasi zaidi ya milioni 13, huku muziki wake ukizidi kuwa na ushawishi mkubwa duniani ukilinganisha na ule wa Diamond.
Wakati Davido akiongoza Afrika, duniani kwa ujumla, mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram ni Selena Gomez kutokea Marekani, na ndiye namba moja pia upande wa wanawake.
Selena aliyeshirikiana na mkali wa Afrobeats kutokea Nigeria, Rema katika wimbo, Calm Down (2022), ana wafuasi milioni 415 tangu ajiunge na Instagram hapo Julai 2013.
Kwa kifupi Selena ameyapita majina makubwa katika tasnia muziki duniani kama Beyonce, Rihanna, Justin Bieber, Madonna, Drake, Jennifer Lopez (J.Lo), Kendric Lamar, Taylor Swift, 50 Cent,.
Haya yanajiri wakati data za Kepios zinaonyesha kuwa hadi kufikia Oktoba 2025, watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani kote walifikia bilioni 5.66. Watu hao bilioni 5.66 hutumia wastani wa saa 18 na dakika 36 kwa wiki wakiwa kwenye mitandao wakitazama picha na video kwenye majukwaa ya Instagram, YouTube, TikTok na Facebook.