ASKARI wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma wametembelea Kituo cha Kulelea Waathirika wa ugonjwa wa Ukoma kilichopo kata ya Litisha Halmashauri ya Songea Vijijini na kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali ili viweze kuwasaidia katika mahitaji yao ya kila siku.

Mkuu wa Kikosi Cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Epimark Mtafi ameongoza askari hao akiambatana na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa huo (ASP) Odiria Mroso na Mkuu wa Kituo Cha Polisi Peramiho (ASP) Mohamed Ngonyani.

Akikabidhi vitu hivyo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma (ACP) Mtafi, amebainisha kuwa Jeshi la Polisi mkoa huo linatarajia kuadhimisha siku ya Familia za askari Polisi (Police Family Day) leo Februari 14, 2026 hivyo wakaona ni vyema kwenda kuwatembelea watu wenye uhitaji na kuwapatia hicho walichojaliwa ili nao wafurahie maisha na kujiona ni sehemu ya jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Ruvuma (ASP) Odiria Mroso amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kama sehemu ya Jamii limekuwa likishirikiana na wanachi katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa pamoja na kuwatembelea watu wenye uhitaji na kuongea nao ili kuwafariji na kuwapatia kile wanachojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Naye Msimamizi wa kituo hicho Sista Daniella Ngonyani amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuona umuhimu wa kwenda kutoa faraja kwa wahitaji hao hivyo amewaomba kuendelea na moyo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *