Rais Xi Jinping wa China ametangaza kuwa, nchi yake itaziondolea ushuru nchi zingine za Afrika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.

Hadi kufikia sasa, China imeshayaondolea ushuru mataifa 33 ya Afrika, huku ikisisitiza kuwa inalenga kuondoa tozo hizo kwa nchi nyingi zaidi barani humo.

Kwa mujibu wa Rais Xi, mpango wa kuziondolea ushuru nchi za Afrika, utatoa fursa kubwa za maendeleo kwa nchi hizo.

Mataifa mengi ya Afrika, kwa sasa yanaiangalia China kama mshirika wao muhimu, baada ya Marekani kuamua kuziwekea nchi za bara hilo viwango vikubwa vya ushuru, mwaka jana.

Hata hivyo msamaha huo hautoihusu Eswatini, nchi ambayo ina uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan.

Hii ni kutokana na kwamba, Beijing imekuwa ikisisitiza kila mara kuwa kisiwa hicho ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya China.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa mchangiaji mkubwa katika maendeleo ya Afrika. Ikiwa ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, nchi hiyo ya Asia Mashariki imekuwa ikitoa msaada wa kifedha na kuwekeza katika miradi ya miundombinu ya Afrika, kama vile ujenzi wa barabara, reli na bandari…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *