
Dar es Salaam. Tanzania na Liberia zimeingia makubaliano ya kihistoria ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya bahari katika maeneo mahsusi ya usajili wa meli, mafunzo kwa mabaharia na kuboresha utendaji wa bandari kwa lengo la kukuza uchumi kupitia sekta hiyo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika hafla fupi iliyofanyika Februari 13, 2026, jijini Dar es Salaam na wawakilishi wa Tanzania na Liberia
Wawakilishi wa mataifa hayo wamesema ushirikiano huo utachochea mabadiliko makubwa katika uchumi wa Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mohamed Salum amesema ushirikiano huo utaiwezesha Tanzania kupata nafasi ya kipekee katika kuimarisha ufanisi wa bandari.
“Kupitia makubaliano haya, maofisa na wafanyakazi wa bahari kutoka Tanzania watafaidika na programu za kubadilishana uzoefu, mafunzo ya kiufundi na fursa za kitaaluma ambazo zitawawezesha kufanya kazi kwenye meli zilizosajiliwa na Liberia.
“Liberia inaongoza duniani katika usajili wa meli, na ushirikiano huu unafungua fursa kubwa za kiuchumi kwa Tanzania,” amesema Salum.
Salum amesema makubaliano hayo yanatoa fursa kwa Tanzania kushiriki katika ajenda na majadiliano ya sera za kimataifa kupitia ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Liberia na Shirika la Bahari la Kimataifa (IMO), licha ya Tanzania kutokuwa mwanachama rasmi wa baraza hilo.
Amesema sekta ya bahari nchini Tanzania inaendelea kukua kwa kasi akitolea mfano bandari ya Dar es Salaam, ambayo awali ilishughulikia tani milioni 17 kwa mwaka, sasa inashughulikia takriban tani milioni 31.
Kupitia Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI), amesema Tanzania imewekeza katika mafunzo ya mabaharia na kuvutia wanafunzi kutoka Kenya, Namibia, Angola, Msumbiji, na Uganda.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Liberia katika Shirika la Bahari la Kimataifa (IMO), Robert Kpadeh ambaye alimwakilisha Kamishna wa Usafiri wa Bahari nchini Liberia, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kihistoria.
“Makubaliano haya yataweka msingi wa urithi ambao vizazi vijavyo vya nchi zetu vitathamini. Afrika kwa sasa inazalisha asilimia 4 pekee ya mabaharia duniani, sawa na mabaharia milioni 1.9.
“Kwa kushirikiana, tunaweza kutoa mafunzo, kuthibitisha, na kuwawezesha kizazi kipya cha wataalamu wa bahari kutoka Afrika,” amesema Kpadeh.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa mataifa ya Afrika unafungua fursa za kukuza uchumi kwa viwango vikubwa.
“Kupitia ushirikiano, uvumbuzi, na kuheshimiana, tunaimarisha utawala wa baharini si tu kwa nchi zetu, bali kwa ustawi wa bara letu. Maendeleo endelevu ya baharini si chaguo, bali jukumu linalotuhusu wote,” amesema.