Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza nini maana ya upendo? Binafsi ninatafsiri upendo kama hisia za kumjali, kumthamini na kumtakia mema mtu au kitu bila kujali yupo katika hali gani, mazingira gani. Kwenye upendo kuna huruma, uaminifu, heshima na kujitoa kwa ajili ya mwingine. Heri ya Siku ya Wapendanao!

Siku hii huadhimishwa  duniani kote kila mwaka ifikapo tarehe kama ya leo, Februari 14. Hupambwa na vitu vingi ikiwemo zawadi,maneno matamu, vitendo vya huruma na mengineo. Wasanii nao hawapo nyuma katika siku hii kwani huitumia kama sehemu ya kujipatia kipato kwa kuachia nyimbo tamu za kusindikiza siku hii maalumu.

Mwaka 2026, mwanamuziki Diamond Platnumz ni kati ya waliotoa kazi mahususi kwa ajili ya Valentine. ‘Natulizana’, wimbo uliotoka siku tatu zilizopita huku staa huyo akiweka wazi kuwa ni kwa ajili ya siku hii muhimu ya wapendanao. Hadi sasa wimbo huo umetazamwa zaidi ya mara laki tano kwenye mtandao wa Youtube

Si Mondi tu mastaa wengi wamekuwa wakiitumia siku hii kama sehemu ya kujiongezea kipato kupita kazi zao. Huku matamasha mbalimbali ya burudani kama lile la mshereheshaji mashuhuri Gara B liitwalo Garaballantine yakiandaliwa kwa lengo la kuwakutanisha wapendanao pamoja.

Licha ya kuwa siku haiwahusu watu walio kwenye mahusiano ya kimapenzi tu. Lakini wao ndiyo huipa kipaumbele zaidi, huku ikigeuka kuwa chachu ya kuimarisha mahusiano yao na kwa wengine valentine hugeuka shubiri kwa kubomoa kabisa mahusiano hayo.

Akizungumza na Mwananchi mwanasaikolojia Christian Bwaya amesema siku hii kwa baadhi ya watu hugeuka ya maigizo.

“Mazoea ya watu wengi ni kujaribu kuonesha kwa watu wengine kwamba wanapendana. Hii huwa siku ya kutambiana kwamba napendwa, mtu atafanya kitu siyo kwa mpenzi wake ni kwa ajili ya watu waone. Ataenda mahali apige picha aposti, utaratibu kama huo hauleti tija, hausaidii wahusika wala watu unaowapostia na kuwatambia.

“Maana ya upendo inapotea inakuwa ni siku ya kuoneshana mimi nimepewa zawadi zaidi. Nimependwa zaidi, mimi ni bora, ikienda kwa mtindo huo haifai. Mfanyie muhusika moja kwa moja badala ya kupostia watu kwanini usipate muda kwa ajili ya kumuonesha mwenzako kuwa unampenda. Hiyo ndiyo maana na huo ndiyo upendo,”amesema

Amesema upendo siyo kwa ajili ya kuwatambia watu. Huku akitolea mfano baadhi ya wapenzi ambao hawaambiani maneno mazuri wakiwa wawili lakini mtandaoni wanaigiza kupendana.

“Hii siku imetafsirika kama siku ya watu kufanya mapenzi. Mimi nadhani ukiangalia historia ya hii siku ililenga kuoneshana upendo. Wale ambao wanawaza kwenda kufanya ngono wanakuwa wameharibu maana ya siku hii. 

“Kupenda haimaanishi mapenzi moja kwa moja. Naweza kumfanyia mtu ambaye siyo mpenzi wangu. Badala ya kuwaza mapenzi na mahaba,onesha upendo kwa watu wenye shida na wahitaji, yatima, wajane, wazee, wafungwa na wagonjwa,”amesema Christian 

Kwa upande wake mtaalamu wa saikolojia, Emelda Mosha amesema kama watu wanavyoadhimisha siku ya wapendanao kwa kupendana ndivyo wanatakiwa kuishi siku zote.

“Maadhimisho siyo kitu kibaya, lakini yawakumbushe kuwa hivyo ndivyo inatakiwa kuwa maisha yao ya kila siku. Pia kuitumua kama siku ya kuboresha mapungufu yaliyo baina yao. Siku hii iwe chachu ya mabadiliko ya suala zima la mahusiano yaliyo baina yao,”amesema.

Emelda ameongezea kuwa mitazamo na matarajio ndiyo kitu kinachopelekea baadhi ya watu kuteteresha mahusiano yao katika siku ya Valentine.

“Wasiigize jaribu kufanya kitu, siyo vibaya kujifunza. Fanya kitu kwa ajili ya mpendwa wako ukimaanisha siyo kwa sababu dunia inataka mfanye hivyo. Siyo lazima kupewa zawadi kwani maisha yenyewe ni zawadi tosha na kuambiana maneno mazuri yanayofanya mtu awe bora zaidi na kujiona wa thamani. Wakati mwingine siyo kitu cha kutoa,” amesema Emelda.

Kwa wafanyabiashara ni neema

Akizungumza na Mwananchi mfanyabiashara wa nguo za kike na kiume kwa njia ya mtandao. Rose Charles amesema tangu kuanza kwa Februari hadi kuelekea siku ya wapendanao, imekuwa mwezi wa neema kwake. 

“Mwezi wa kwanza ulikuwa mgumu sana kwangu kibiashara. Ilikuwa zinapita hadi siku mbili bila ya kuuza chochote lakini tangu shamrashamra za siku ya wapendanao kuanza biashara imekuwa nzuri,”ameeleza.

Rose amesema katika kipindi cha kuelekea siku hii ya maadhimisho ya wapendanao aliuza sana tisheti maalumu, ambazo zinakuwa zimeandikwa jumbe mbalimbali za upendo.

“Kila tisheti moja ninauza kwa Sh20,000 na nilinunua mzigo wa tisheti za aina hiyo takribani 40 na hadi kufikia jana zote zilikuwa zimeisha. Huku wateja wengine wakipiga simu kuziulizia,”amesema .

Picha ya wapendanao. Imetengenezwa na Akili Mnemba

Naye Betna John ambaye anajishughulisha na uuzaji wa keki amesema msimu wa Valentine mwaka huu biashara imekuwa nzuri haswa kwa keki kwa ajili ya wapendanao.

“Kwa siku tatu zilizopita biashara imeanza kuchangamka. Nilipokea simu na wengine kufika ofisini kwa ajili ya kuweka oda za keki kwa siku ya leo kupeleka kwa wawapendao.

“Siku za kawaida kama hakuna maadhimisho yoyote huwa napokea oda moja au mbili kwa siku. Lakini siku hizi za karibuni napokea oda za keki tano hadi saba,” amesema.

Aidha Mwanaidi Nassoro ambaye anajishughulisha na uuzaji wa maua katika eneo la Mbuyuni jijini Dar es Salaam, amesema msimu huu wa Valentine biashara siyo nzuri sana kutokana na kupanda kwa bei ya maua shambani.

Mwanaidi amesema inawalazimu kuongeza bei ili waweze kutengeneza faida. Jambo linalopelekea baadhi ya wateja kushindwa kununua bidhaa hiyo.

Ameeleza moja ya sababu iliyopelekea kuongezeka kwa bei ya maua shambani ni pamoja na kuongezeka kwa mahitaji yake haswa katika huu wa siku ya wapendanao.

“Kwa sasa ua moja ambalo awali lilikuwa likiuzwa Sh2000. Sasa linauzwa kuanzia Sh3000 hadi Sh3500 kwa moja,”amesema.

Naye dereva wa teksi mtandao, Almasi Matata amesema inapokaribia sikukuu ya wapendanao, huwa anapata safari nyingi tofauti kwa kuwa watu hupenda kuwapeleka wapendwa wao sehemu tofauti.

Historia ya siku hii

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya historia ya www.countryliving.com, wakati wa karne ya tano kulikuwa na kiongozi aliyeitwa Mfalme Claudius II ambaye aliamini askari anapooa hawi mkakamavu na pia muda mwingi anawaza kuhusu familia yake, zaidi ya kitu kingine chochote.

Hivyo, alipiga marufuku ndoa kwa askari. Kitendo hicho hakikuwafurahisha watu wengi, akiwamo Padri Valentino. Kiongozi huyo wa kidini aliendelea kufungisha ndoa kwa siri.

Mfalme Claudius alipopata habari hizo aliamuru Padri Valentino akamatwe na kuuawa.
Mtakatifu Valentino aliuawa Februari 14, ndiyo maana ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama baba wa upendo na mtetezi wa wanandoa. Historia inaonyesha kuwa aliyetangaza kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius.

Pia, ipo simulizi nyingine inayosema akiwa gerezani kwa amri ya Mfalme Claudius, Padri Valentino aliandika barua iliyokuwa na salamu kwa binti aliyekwenda kumsalimia gerezani mara kwa mara kabla ya hukumu ya kifo chake. Mwisho wa barua alihitimisha kwa kusema ‘Kutoka kwa Valentino wako’. Tangu hapo, Valentino anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake huadhimishwa ulimwenguni kote.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, baadaye, Padri Valentino alikuja kutangazwa kuwa Mtakatifu.

Mitazamo ya watu kuhusu siku hii

Akizungumza na Mwananchi Gaudensi Franco mkazi wa Chanika, Jijini Dar es Salaam amesema siku hii haimaanishi kitu chochote kwake.

“Unajua tunatakiwa kupendana kila siku na siyo kwenye Valentine tu. Lakini watu wanasahau sana wengi siku hii ndiyo wanapeana maua na zawadi nyingine, lakini baada ya hapo chuki wanaziendeleza hii haifai na ndiyo maana mimi naichukulia siku hii kama siku nyingine,”amesema

Aidha Salumu Mustafa mkazi jijini humo amesema Siku ya Wapendanao ni muhimu kwa sababu inawakumbusha watu kuonyesha upendo .

“Sio kila siku watu hupata muda wa kuambiana ‘nakupenda’ au kutoa zawadi. Naipenda Valentine kwa sababu inasababisha furaha na mshikamano. Migahawa, hoteli na wafanyabiashara wengine hujiingizia kipato zaidi siku hii,”amesema 

Naye Bhoke Mwita mkazi wa Kitunda amesema Valentine imegeuka kuwa siku ya biashara zaidi kuliko kuoneshana upendo. Watu wanalazimika kununua zawadi za thamani ili kuthibitisha mapenzi yao, jambo ambalo si la lazima.

“Siku hii huleta presha kwa watu wasio kwenye mahusiano. Na wengine hujihisi wapweke. Kinachokera ni baadhi ya watu kusahau kuadhimisha siku hii na watu wenye uhitaji,” ameeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *