Dar es Salaam. Serikali imesema programu ya kuwajengea uwezo maofisa wa mifugo katika utambuzi, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya wanyama (ISAVET) ni muhimu kwa kulinda sekta ya mifugo, inayobeba maisha ya Watanzania wengi vijijini na mijini.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 14, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dk Semvua Mzinghani, wakati akifunga mafunzo ya wataalamu wa mifugo yaliyoendeshwa kwa ushirikiano wa Serikali na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia programu ya ISAVET.

Amesema mafunzo hayo yanawapatia wataalamu ujuzi wa vitendo wa kugundua magonjwa ya mifugo mapema kabla hayajageuka milipuko mikubwa, hatua inayosaidia kulinda uzalishaji, biashara ya mifugo na afya ya jamii.

“Mafunzo ya ISAVET yanawawezesha wataalamu kutambua magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo na kuchukua hatua za kudhibiti kwa wakati. Tafiti zinazofanywa kupitia programu hii pia zinaisaidia Serikali kupanga mikakati kwa kuzingatia changamoto halisi zilizopo mashambani,” amesema Dk Mzinghani.

Wahitimu wa mafunzo wakiwa na mgeni rasmi pamoja na viongozi wengine wa FAO katika picha ya pamoja.

Amesisitiza kuwa ushahidi wa kitaalamu unaokusanywa na wahitimu hao katika mazingira ya ufugaji unatoa mwongozo muhimu kwa Serikali katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya milipuko.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa FAO nchini, Dk Nyabenyi Tipo, amesema mahafali hayo si mafanikio ya washiriki pekee bali ni hatua ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya afya ya wanyama nchini.

Amesema sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika maisha ya watu, usalama wa chakula, lishe, biashara na afya ya umma, lakini bado inakabiliwa na changamoto za magonjwa yanayoibuka na kurejea, mabadiliko ya tabianchi, minyororo ya thamani inayopanuka, magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na usugu wa viuatilifu.

Ameonya kuwa kuchelewa kugundua milipuko ya magonjwa husababisha athari kubwa kwa kaya na masoko, na hata kutishia usalama wa afya ya taifa. Amesema FAO inaunga mkono azma ya Tanzania kupanua ISAVET kuwa sehemu ya msingi ya maendeleo ya rasilimali watu katika sekta ya afya ya wanyama kwa kuimarisha mafunzo ya darasani, miradi ya shambani na mfumo wa uanagenzi.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Goodluck Osha, amesema ujuzi walioupata utasaidia kutatua changamoto za magonjwa ya mifugo kwa wafugaji na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Sherehe hiyo iliwakutanisha maofisa wa serikali, washirika wa maendeleo na wataalamu wa mifugo, wakiahidi kuendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa kwa kuzingatia mkakati wa One Health unaounganisha afya ya wanyama, binadamu na mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *