Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Mkutano wa Usalama wa Munich uliokua na mtazamo dhidi ya Iran umegeuka na kuwa kongamano la sakarakasi na hivyo kudhihirisha namna Ulaya ilivyopoteza ushawishi wake wa kijiopolitiki na umuhimu wa kistratejia.

Araqchi jana alituma jumbe kadhaa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akisema kwamba: “Inasikitisha kuona Kongamano kubwa la Usalama la Munich likigeuzwa kuwa ‘Sarakasi ya Munich’  linapokuja suala la Iran.” 

“EU inaonekana kuchanganyikiwa; kimsingi Umoja wa Ulaya umepoteza ushawishi wake wa kijiopolitiki katika ukanda wetu,” amesema Abbas Araqchi.

Mkutano wa Usalama wa Munich, Ujerumani ambao kila mwaka huhudhuriwa na waku wa nchi, mawaziri wa mambo ya nje, maafisa wa kijeshi na wataalamu wa sera, unatambulika kama jukwaa kuu la dunia la kujadili changamoto za usalama duniani.

Mkutano wa mwaka huu ulikuwa na mijadala kuhusu vita vya Ukraine, Iran na mivutano katika Bahari ya Antlantiki. Hata hivyo majopo ya Iran yalikabiliwa na maneno makali. Washiriki kadhaa katika mkutano huo walitoa wito wa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran.

Miongoni mwao ni mwana wa kiume wa Shah Reza Pahlavi, mfalme aliyefukuzwa na wananchi wa Iran, ambaye alitumia jukwaa hilo kuunga mkono mashinikizo yanayoongezeka na hata mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Tehran.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa kudhoofika kwa msimamo wa Umoja wa Ulaya kunadhihirika katika juhudi zinazoendelea za kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwamba Ulaya, ambayo hapo awali ilizingatiwa kama mpatanishi muhimu katika diplomasia ya nyuklia, sasa haina nafasi yoyote muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *