
Dar es Salaam. Leo tuongee kidogo na GenZ wanaoota kama masupastaa lakini wanalala kama mbwa koko. Namaanisha wanaoota pepo wakiwa jehanamu. Mifano yangu isiwatishe manake nakosa namna nzuri ya kusema, lakini twende pamoja na utanishukuru baadaye.
Kuna dogo yupo mtaani, ana kipaji na anatembea na mistari hata Mbosso akasome. Lakini huyu dogo kila akipambana, anajikuta akipiga hatua moja mbele na kurudi hatua nne nyuma. Anahisi labda anabaniwa, au zaidi anaona kama aliyepuliziwa upepo mchafu na wenzie.
Kitu ambacho madogo hawakijui, muziki ni pesa. Kuzitafuta pesa ni lazima uwe na pesa. Huwezi kuandika nyimbo kali wakati unafikiria hela ya kula. Wala huwezi kuendelea iwapo unaziuza nyimbo hizo kulipia kodi ya nyumba.
Usiulize mbona wanamuziki wa zamani walikuwa masikini lakini wakatoka. Muziki ule na muziki huu ni tofauti kabisa. Ule haukuwa wa kibiashara kwa mwanamuziki mmoja mmoja.
Lakini sio kweli kwamba fani zao hazikuwalipa. Mbaraka Mwinshehe alipata ajali akiwa safarini kwenda kurekodi Kenya. Yeye alimiliki gari ingawa kwa siku hiyo alisafiri kwa gari ya swahiba wake. Wakati huo mfanyakazi wa kiwango cha kati wa Serikalini asingeweza kuota kumiliki Peugeot 404 hata kwa mkopo.
Dj Kalikali alikuwa na chumba pale Kilimanjaro Hotel. Alikuwa akipelekwa kazini YMCA na Mercedes Benz. Hata mkisema aliwezeshwa na tajiri wake, mzee Mbowe, hiyo si ndiyo maana ya mikataba? Mnaujua uhusiano wa Diamond Platinumz na Wasafi TV, Diamond Karanga na Chibu Perfume?
Hata vijana walioshuhudia mwanzo wa muziki wa kizazi kipya waliona ukaribu uliokuwepo baina ya muziki na ukwasi. Mnakumbuka muziki huu ulipanda kwa kasi kule makochini zaidi ya uswazi. Kama mnawajua Kwanza Unit, wote walikuwa ni watoto wa watu wenye uwezo.
Wengine baba zao walifanya kazi za kibalozi na kimataifa. Wengine walikuwa wafanyabiashara wakubwa walioweza kujijenga katika maeneo ghali kama Oysterbay, Upanga, Masaki na kadhalika. Watoto hawa waliweza kulipia gharama za studio kwa kujichanga ama kusaidiwa na wazee wao.
Mimi nilipata kuishi kwenye kota za Serikali za Chang’ombe Maduka Mawili. Tulijiona tukiwa ushuani kwani tulipakana na uswazi (Toroli na Unubini), lakini hadhi ya nyumba zetu ilikuwa ya chini kulinganisha na zile za Oysterbay. Kule kota zao zilikuwa za mabosi akiwemo Waziri Mkuu.
Hivyo pamoja nao kuwa na uswazi yao, maisha yalitofautiana kulingana na fursa. Uswazi ya kwao ilikuwa karibu sana na fursa ukilinganisha na uswahilini yetu. Dogo wa kule aliweza kumwonesha maujuzi mtoto wa bosi, naye akayaona maujuzi hayo kuwa ni tiketi kwao wote wawili.
Huku kwetu TMK kulikuwa na vipaji vingi sana kama ilivyokuja kuonekana baadaye. Lakini mwanzoni mtoto wa uswazi aliyetaka kutoboa kimuziki ilimlazimu kwenda kujichanganya Oysterbay au Masaki, kisha aletwe katika Studio ya Henrico iliyokuwepo palepale Chang’ombe.
Hapo ndipo utajua kuwa kuishi msikitini hakumaanishi kuswali. Yaani Studio ipo palepale lakini namna ya kuingia ilibidi ukaitafute Upanga! Lakini jambo hilo sio la ajabu katika kusaka fursa. Unaweza kutoka Dar ukaisogelea fursa Dodoma.
Msimwone Chibu kama mtu wa ajabu sana kwa kuwa maarufu na ana fedha. Yeye alipigania alichokitaka. Tangu mwanzoni alijieleza kuwa alitamani fedha na umaarufu, akapambania ndoto zake. Hivyo jambo la kwanza ni msanii kujua anataka kutoboa ili iweje.
Jambo la pili ni uwekezaji. Watu wanaofanikiwa ni wale ambao wanaunganisha rasilimali zao. Ni nadra sana kuona mtu ana kila kitu kitakachomfikisha kwenye matarajio yake. Awe na kipaji, awe na fedha na aweze kujitangaza. Zingatia kuwa wabunifu wengi huwa ni wale wasio na kitu.
Labda hii inafanana na mtu anayebuni kugeuza taka kuwa nishati. Ni lazima afanye utafiti wa namna ya kuzikusanya taka hizo, awe na nyenzo za kuzigeuza kuwa nishati na namna ya kuutangazia umma, kwa maana ya kutafuta masoko. Hana budi kuwashirikisha watu wenye fedha na wa matangazo.
Raslimali hizi tatu zikiunganishwa mafanikio ni lazima yatokee. Kama vile tulivyoona watoto wa Upanga walivyotoboa, vivyo hivyo watoto wa TMK wakatoboa. Walizifuata fursa kule zilipo na mambo yakawa utelezi. Tena hili si kwa hapa nyumbani tu, bali mambo haya yanafanyika kote duniani.
Wasanii wote wakubwa waliwekeza kwenye vipaji vyao. Nikimnukuu Diamond, aliwashawishi watu waliowekeza kwenye utangazaji, akaingia ubia na kumiliki kituo cha TV. Msije kudhani alichota pesa za albamu na kuanzisha miradi mipya. Hata akina Jay Z nao wanafanya michakato kama hii.
Marekani ina wasanii wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kuna Waarabu, Wachina, Waafrika na kadhalika. Hata kama wenyeji hawana vipaji vya sanaa, lakini wana majiji makuu kama Hollywood ambayo yana kila kinachohitajika kwenye sanaa. We nenda na kipaji, fedha na matangazo utayakuta huko.
Unaambiwa taa haiwashwi na kuwekwa uvunguni. Mkiendelea kufanya sanaa chumbani, mtajaza makaunta ya mistari, na mtazeeka mkiwasaka wachawi. Hata kama studio imepangishwa kwenye nyumba ya babaako utaitazama kwa macho tu. Lakini mkitafuta wabia mtacheka kizungu mkiwa kando ya mabwawa yenu ya kuogelea.