Chama Cha Mafundi Tanzania (CMT), Joseph Kusaga Foundation na Unicx AI Data Limited zimeingia ubia mpya wa kimkakati unaolenga kubadilisha sekta ya mafundi Tanzania kupitia teknolojia, huduma za kifedha na fursa za kidijitali.
Makubaliano hayo yaliwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Unicx AI Data, Noel Mangoma, pamoja na Mwenyekiti wa CMT, Humfrey Mtenda, yakilenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa mafundi, kufungua masoko ya kidijitali, na kujenga mfumo wa kitaifa wa data na utambulisho wa kitaaluma kwa kila fundi.
Ushirikiano huo pia utaunganisha mafundi moja kwa moja na taasisi za kifedha pamoja na washirika wa maendeleo, hatua itakayoongeza uwezo wao kiuchumi na thamani ya ujuzi pamoja na huduma zao.
Zaidi ya kuwa ushirikiano wa kawaida, hatua hii inaashiria mwanzo wa mabadiliko ya kiuchumi kwa mafundi Tanzania — yakichochewa na teknolojia, uaminifu, fursa na ukuaji.
