DODOMA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sanga amezindua Mkakati wa Kukuza Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Nyumbani 2025/26 – 2029/2030 kwa lengo la kuwahakikishia wafanyakazi wa nyumbani wanapata ulinzi, kutambuliwa na kupata fursa wanazostahili ili kukuza kazi za staha.

Mbali na uzinduzi wa mkakati huo pia Waziri Sanga amezindua programu ya Nchi ya Kazi za Staha Awamu ya Tatu kwa mwaka 2025/26 – 2029/2030.

Akizungumza hayo jana mkoani Dodoma katika uzinduzi wa Programu na Mkakati huo, Waziri Sangu alisema kwa upande wa programu hiyo inalenga kuimarisha majadiliano ya kijamii na mshikamano baina ya Serikali, waajili na wafanyakazi .

Alisema kwa upande wa mkakati huo ambao ni wa kwanza kwa nchi ya Afrika kuzinduliwa utahakikisha wafanyakazi wa nyumbani wanapata ulinzi na kufikiwa na fursa wanazostahili ili kuongeza kazi za staha.

”Natoa shukrani kwa Shirika la Kazi Duniani ILO ambalo limeendelea kushirikiana nasi kutoa msaada wa Kitaalam na Kifedha kufanikisha kuzinduliwa kwa mkakati huu na programu hii ya nchi ya kazi ya staha na mkakati wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani,”alisema

Waziri Sangu alisema nchi ya Tanzania imekuwa mwanachama wa ILO tangu mwaka mwanzoni mwa mwaka 1960 hadi sasa nchi imeridhia mikataba 37 ya Shirika hilo ikiwemo mikataba nane ya misingi.

”Serikali inaendelea kutekeleza mikataba hiyo kupitia sera,sheria na taratibu zinazotolewa na mamlaka mbalimbali hatua hiyo inalengo kuimarisha na kukuza uzingatiaji wa masuala ya kazi za staha nchini,”alisema.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Kazi,Suzan Mkangwa alisema Serikali inaenda kutekeleza Mkakati na Programu hiyo kwa kuzingatia kazi za staha kwa kuhakikisha wafanyakazi wote nchini wanakuwa na kazi za staha.

”Leo tumezindua mkakati wa kusaidia wafanyakazi wa nyumbani ambao unalenga kuimarisha kazi za staha katika kundi la wafanyakazi wa nyumbani na ni hatua kubwa ya nchi kuelekea njia ya kuridhia mkataba wa ILO namba 189 .

”Ndani ya Mkakati hiyo kuna mambo mbalimbali ambayo yatasaidia kwa namna moja au nyingine kusimamia utekelezaji wa sheria kwenye eneo hili la wafanyakazi wa nyumbani.

”Nchi ipo katika hatua mbalimbali za kuridhia Mkataba wa ILO kuhusiana na Wafanyakazi wa nyumbani hivyo kama serikali tayari tumetengeneza kanuni katika eneo hili la wafanyakazi wa nyumbani hii yote ikiwa ni maandalizi ya kuridhia Mkataba huu,”alisema

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani(ILO)Afrika Mashariki,Caroline Mugala alisema kazi za staha ni utu hivyo jambo jema kwa nchi wananchama wa ILO ni kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi za staha kwa kuwa zinahakikisha haki katika maeneo ya kazi,kinga ya jamii na majadiliano memo katika maeneo ya kazi.

”Ni kweli mradi wao wa Kukuza Utambuzi na Kuboresha Mazingira ya Kazi kwa Wfanyakazi wa Nyumbani unaelekea kuisha lakini Kazi inaendelea,katika miradi yote lazima iwe na mwanzo na mwisho lakini kazi ambayo imeanzishwa na mradi huu ndio inaanza.

”Hivyo kama kazi inaelekea kuanza tunaona namna Mkataba wa ILO unaelekea kuridhiwa na kupitia jitihada hizi tunaona hata wengine kuja kujifunza mafanikio ya programu,”alisisitiza

Elizabeth Rafael ni Mmoja wa Wafanyakazi wa Nyumbani ambaye amehitimu Chuo cha VETA,alisema mkakati uliozinduliwa utawasaidia wao kama wafanyakazi wa nyumbani kuwapa kinga,kupata mikataba ya ajira kwa maandishi tofauti na awali kwa mdomo na kupelekea kuwa chachu kwa serikali kuridhia mkataba wa ILO namba 189 .

”Tumefurahia sana kuwa hapa kuzinduliwa kwa hii programu ambayo itakuwa msaada mkubwa kwetu,”alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *