KLABU ya Al Ahli Tripoli ya Libya inayoshiriki Ligi Kuu ya Libya, ipo hatua ya mwisho kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa RS Berkane ya Morocco na timu ya Taifa ya Senegal, Mamadou Lamine Camara, ikiwa ni ishara nzuri kwa kikosi cha Azam FC iliyokuwa na presha na kumpoteza Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Matajiri hao wa Libya, walikuwa wakimpigia hesabu za kumng’oa kiungo mshambuliaji huyo nyota wa Azam, Fei Toto kwa muda mrefu, ingawa licha ya kiasi kikubwa cha fedha kilichowekwa, matajiri hao wa Chamazi hawakukubali aondoke.

Sababu kubwa iliyowafanya mabosi wa Azam kumzuia Fei asijiunge na matajiri hao wa Libya katika dirisha dogo la Januari, ni kutokana na michuano muhimu ambayo timu hiyo inashiriki ikiwamo Kombe la Shirikisho Afrika ambapo usiku wa jana ilikuwa Morocco kuumana na Wydad AC ikisaka tiketi ya robo fainali.

Tripoli iliweka kiasi cha Sh4.5 bilioni ili kumpata nyota huyo ambaye amekuwa na mwendelezo mzuri akiwa na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, tangu alipojiunga nayo mwaka 2023, akitokea kwa mabingwa watetezi wa Ligi, Yanga.

Usajili wa Camara, huenda ukaipa Azam utulivu wa kuendelea kubakia na Fei Toto hata kwa msimu ujao kutokana na umuhimu wake kikosini, licha ya awali kuhusishwa pia kurejea Yanga, sambamba na Simba na miamba ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs.

Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimzidi, Stephane Aziz KI aliyekuwa anaichezea Yanga kwa wakati huo, aliyefunga 12 na kuasisti tisa.

Mwaka 2024, Fei aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi, akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad SC ya Libya, ambapo hadi anaondoka alichangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa.

Kiwango bora cha Fei kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI aliyekuwa Yanga aliyefunga mabao 21.

Pia, alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2023-2024, kwa kuifikisha Azam fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5 baada ya suluhu ya (0-0) ya dakika 120 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Juni 2, 2024.

Mbali na hilo pia, Fei aliiwezesha Azam kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 10, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kiliposhiriki mwaka 2015, kufuatia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2013-2014.

Timu hiyo ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024-2025, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara kwa pointi 63, hata hivyo, kikosi hicho kiliishia hatua ya awali, baada ya kuondolewa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1.

Msimu wa 2024-2025, Fei alichangia mabao 17 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mabao manne na kuasisti 13, huku pia akiiwezesha Azam kuandika rekodi mpya ya kufuzu hatua ya makundi ya Michuano ya CAF, tangu ilipoanzishwa Julai 23, 2004.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *