Marekani. Msanii wa Hip-Hop kutokea Marekani, Cardi B, (33), anajiandaa kuingia rasmi kwenye soko la bidhaa za nywele hivi karibuni, ikiwa ni baada ya kuzindua chapa yake mpya ya urembo, Grow-Good Beauty.
Mradi huo (Grow-Good Beauty) ni sehemu ya ubia kati ya Cardi B na kampuni ya Revolve Group, ambao ni wauzaji mkubwa wa bidhaa za mitindo na urembo ikiwa na makao yake California.
Kupitia makubaliano hayo ambayo yamepokelewa vizuri na mashabiki wake, pande hizo mbili zinashirikiana katika uwekezaji wa bidhaa za mavazi na urembo.
Hata hivyo, hii ndio mara ya kwanza kwa Cardi B kumiliki moja kwa moja chapa yake binafsi ya urembo, hatua inayodhihirisha kukua kwake kibiashara nje ya muziki.
Cardi B alitangaza habari hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram, huku akijiandaa kuanza ziara yake iitwayo ‘Little Miss Drama’ itakayoanzia huko Palm Desert, California.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe kubwa na wafuasi wake mtandaoni, huku wengi wakionesha hamu ya kuona bidhaa atakazokuja nazo sokoni.
Kwa muda mrefu sasa, mashabiki kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakishuhudia namna Cardi B amekuwa akizitunza nywele zake za asili, na sasa anataka kupiga hatua zaidi katika eneo hilo.
Mara kadhaa amewahi kuposti video mtandaoni akionyesha jinsi anavyoosha nywele zake, hatu za ukuaji wake, pamoja na mbinu mbalimbali za kurutubisha nywele anazotumia nyumbani kwake.
Aliwahi kueleza kuwa baada ya miaka mingi ya kutumia kemikali, rangi na vifaa vya moto vilivyoharibu nywele, aliamua kuchukua hatua ya makusudi ya kutunza nywele kwa njia asilia zaidi.
Licha ya mara kwa mara kuonekana akiwa na wigi, Cardi B ameonyesha kuwa nywele zake za asili ni ndefu, nzito na zenye kuvutia, zikishuka hadi mgongoni. Hatua hiyo imewapa mashabiki wengi hamasa ya kutaka kufahamu siri ya mafanikio yake katika utunzaji wa nywele.
Tangu alipovuma kupitia wimbo wake, Bodak Yellow (2017) uliotikisa dunia, Cardi B amekuwa akipiga hatua kubwa si tu kwenye muziki bali pia kwenye biashara na mitindo.
Albamu yake ya kwanza, Invasion of Privacy (2018) ilimletea tuzo ya Grammy, na tangu hapo ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni zaidi ya msanii wa kawaida.
Katika safari yake ya ujasiriamali, amewahi kushirikiana na kampuni mbalimbali zikiwemo Fashion Nova, Reebok na NYX Professional Makeup. Vilevile, amewahi kuwa balozi wa chapa kubwa kama Skims, Marc Jacobs na Balenciaga.