Riyadh, Saudi Arabia. Cristiano Ronaldo jana alifunga bao dakika ya 18 tu katika mechi yake ya kurejea akiwa na Al-Nassr, akimaliza ukame wa mechi tatu bila kufunga uliotokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kutoridhishwa kwake na uongozi wa klabu hiyo.
Nyota huyo wa Ureno, anayetimiza miaka 41 mwezi huu, aliipatia timu yake uongozi wa 1-0 ugenini dhidi ya Al-Fateh katika mchezo muhimu wa mbio za ubingwa wa Saudi Pro League.
Al-Nassr iliingia katika mechi hiyo ikiwa nafasi ya tatu, pointi nne nyuma ya vinara Al-Hilal, ambao walimsajili Karim Benzema katika dirisha la hivi karibuni la usajili.
Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kuongoza katika ushindi wa 2-0 kwenye Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi Al Fateh. Picha na Mtandao
Hata hivyo, Ronaldo hakuonyesha presha yoyote alipounganisha kwa shuti la voli krosi ya Sadio Mané na kisha kukimbilia kona kusherehekea kwa mtindo wake maarufu wa “Siu”, jambo lililowasisimua mashabiki waliokuwa uwanjani.
Bao hilo limenfanya Ronaldo afikishe katika jumla ya mabao 962 katika maisha yake ya soka, akibakiwa na mabao 38 tu kufikia lengo lake la mabao 1,000. Bado anaendelea kufunga kwa kasi kubwa, akiwa tayari amefunga mabao 19 katika mechi 23 msimu huu.
Ronaldo alivaa kitambaa cha unahodha na bado anaungwa mkono na mashabiki wa klabu hiyo licha ya kukosa mechi tatu, mashabiki walikuwa wakipeperusha bendera kwa heshima yake wakati alipokuwa nje ya kikosi.
Bao lake lilikuja huku akilipwa takribani pauni 488,000 kwa siku, na ripoti zikidai kuwa alikuwa amekasirishwa na matumizi madogo ya Al-Nassr katika usajili ukilinganisha na wapinzani wao. Tangu msimu wa 2022-23 alipowasili, wapinzani wao wa ubingwa, Al-Hilal, wametumia kiasi cha pauni 180 milioni zaidi ya Al-Nassr.
Hali hiyo ipo licha ya kwamba Al-Nassr, Al-Hilal, Al-Ittihad na Al-Ahli zote zinamilikiwa kwa sehemu kubwa na Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF).
Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kuongoza katika ushindi wa 2-0 kwenye Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi Al Fateh. Picha na Mtandao
Kumrejesha Ronaldo kikosini ni jambo la kutia nguvu kwa Al-Nassr na pia kwa mamlaka za soka za Saudi Arabia, ambazo zinataka ligi yao ionekane ya kuvutia zaidi kimataifa. Hali mbaya zaidi kwao itakuwa iwapo Ronaldo ataondoka kabla ya mkataba wake kumalizika mwaka 2027.
Mwezi Desemba, Ronaldo alidokeza kuwa huenda akamalizia soka lake kwingineko akisema: “Nina shauku kubwa na nataka kuendelea. Haijalishi ninacheza wapi, iwe Mashariki ya Kati au Ulaya.”
Katika taarifa iliyotolewa kwa Daily Mail Sport, uongozi wa ligi ulisema kuwa malalamiko ya Ronaldo hayakuwa na msingi. “Saudi Pro League imejengwa katika kanuni rahisi: kila klabu inafanya kazi kwa kujitegemea chini ya sheria zilezile,” walisema.
“Vilabu vina bodi zao, watendaji wao na uongozi wao wa soka. Maamuzi kuhusu usajili, matumizi na mikakati hufanywa na vilabu vyenyewe, ndani ya mfumo wa kifedha ulioundwa kuhakikisha uendelevu na ushindani wa haki. Mfumo huo unatumika sawa kwa vilabu vyote.
“Cristiano amekuwa akijihusisha kikamilifu na Al-Nassr tangu alipowasili na amechangia pakubwa katika ukuaji na matarajio ya klabu. Kama mshindani wa kiwango cha juu, anatamani kushinda. Lakini hakuna mtu mmoja, hata awe muhimu kiasi gani anayefanya maamuzi nje ya klabu yake.”
Msemaji huyo aliongeza kuwa shughuli za hivi karibuni za usajili “zimeonyesha wazi uhuru huo.”