Dar es Salaam. Ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuimarisha sekta ya kilimo nchini, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inashiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo yanayofanyika nchini Qatar.
Ushiriki wa maonesho hayo yaliyoanza Februari 12 hadi 16,2026 unaonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa na yenye tija. Kushiriki katika jukwaa la kimataifa kama hilo kunatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, teknolojia na mbinu bora za kilimo kutoka mataifa mbalimbali.
Maonesho hayo yanawakutanisha wadau kutoka nchi tofauti, wakiwemo wawekezaji, taasisi za kifedha za maendeleo, wataalamu wa teknolojia za kilimo, wasambazaji wa pembejeo na watunga sera.
Akizungumza leo, Februari 15, 2026, akiwa Qatar katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri, amesema ushiriki huo ni fursa adhimu ya kujenga mitandao ya kimkakati itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha na utaalamu kwa ajili ya kukuza kilimo nchini Tanzania.
“Ushiriki wetu katika maonesho haya ni hatua muhimu ya kufungua milango ya ushirikiano mpana wa kimataifa. Tunataka kuhakikisha TADB inajifunza kutoka kwa wenzetu, inavutia uwekezaji na inawaunganisha wakulima wa Tanzania na fursa za masoko ya kimataifa,” amesema Mkani .
Amepongeza “Kupitia majukwaa kama haya, tunaimarisha uwezo wetu wa kifedha na kitaalamu ili kuifanya sekta ya kilimo iwe ya kisasa, himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi na yenye ushindani katika soko la dunia.” amesema
Mkani amesema ni muhimu uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa kama kilimo cha kidijitali.
“Benki yetu inaamini kuwa ushirikiano wa kimataifa unaweza kusaidia kufungua masoko mapya ya nje, hususan katika ukanda wa Mashariki ya Kati.,” amesema
Kwa upande wake, Meneja Masoko na Mahusiano wa taasisi hiyo, Irene John, amesema pamoja na kupanua wigo wa ushirikiano kimataifa, TADB inalenga kuhakikisha wakulima wa Kitanzania wananufaika moja kwa moja na fursa hizo.
“Lengo letu si kushiriki tu, bali kuhakikisha matokeo ya ushiriki huu yanaonekana kwa wakulima wetu. Tunataka wapate mitaji nafuu, teknolojia sahihi na masoko ya uhakika yatakayowaongezea kipato na kuboresha maisha yao,” amesema Irene John.
Amesema ushiriki wa TADB katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo nchini Qatar ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
“Ni ishara ya dhamira ya benki yetu katika kuleta maendeleo endelevu na kuchochea uchumi wa taifa kupitia kilimo chenye tija na ushindani.,” amesema John