KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amepokea ombi la Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, la kuitaka Serikali kuipandisha hadhi Nzega kuwa mkoa, na kuahidi kulifikisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani, Nzega Mjini mkoani Tabora, Kihongosi amesema hoja ya kuifanya Nzega kuwa mkoa inaungwa mkono na vigezo vya msingi, ikiwemo idadi kubwa ya watu, ukubwa wa eneo pamoja na uwezo wa halmashauri kujitegemea kiutawala na kifedha. Amesema ombi hilo linakuja wakati Nzega ikiendelea kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.
Kihongosi ametaja ujenzi wa mabweni mapya ya kisasa, upanuzi wa shule hadi kidato cha tano na sita, ujenzi wa hospitali ya wilaya yenye vifaa tiba vya kisasa pamoja na maendeleo ya Chuo cha VETA Nzega kuwa ni vielelezo vya ukuaji wa kasi wa eneo hilo. Alisisitiza kuwa maendeleo hayo yanaongeza uzito wa hoja ya Nzega kupewa hadhi ya mkoa. “Nimelipokea ombi hili kwa niaba ya chama na nitalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wetu,” alisema Kihongosi.

Kwa upande wake, Bashe ameiomba Serikali kuipandisha hadhi Nzega kuwa mkoa, akieleza kuwa eneo hilo lina vigezo vya kutosha kiutawala, kiuchumi na kijamii. Amesema idadi ya watu katika eneo la Nzega, akijumuisha majimbo ya jirani ya Igunga na Manonga pamoja na halmashauri zake, inafikia zaidi ya milioni 1.8, jambo linaloonyesha ukubwa na umuhimu wake kitaifa.
Bashe ameeleza kuwa Nzega ina miundombinu inayokua kwa kasi, ikiwemo barabara za lami, masoko, vituo vya mabasi, hospitali na miradi mingine ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa. Amebainisha kuwa Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya ujenzi na upanuzi wa huduma za kijamii, hatua inayoonyesha kuwa Nzega inaendelea kupiga hatua kubwa kimaendeleo. Alisema kupandishwa kuwa mkoa kutasaidia kuratibu na kusimamia maendeleo hayo kwa ufanisi zaidi.

Aidha, aligusia umuhimu wa kuanzishwa kwa Halmashauri ya Ndala na kuimarishwa kwa Halmashauri ya Bukene ili kupunguza usumbufu wa wananchi kufuata huduma mbali, akisema miundombinu ya awali ipo na kinachohitajika ni uamuzi wa kisera ili kusogeza huduma za kiutawala karibu na wananchi.
Amesisitiza kuwa Nzega ni kitovu cha wakulima na wafugaji, hivyo kuwa mkoa kutachochea zaidi ukuaji wa uchumi wa kilimo na mifugo. Ameeleza kuwa hadhi ya mkoa italeta fursa zaidi za uwekezaji, ajira na uboreshaji wa miundombinu ya biashara, na hivyo kuongeza mapato ya ndani na ya taifa kwa ujumla.
Vilevile, Bashe aliomba salamu zake zifike kwa Rais Samia, akisema wananchi wa Nzega wana imani na uongozi wake na wanaamini ombi lao litazingatiwa kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla. SOMA: Kihongosi : Ujenzi wa Sekondari Puge Ukamilike Machi