BAGAMOYO: Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT) kimeiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuwasaidia wajane kwa kuwapatia mitaji na vitendea kazi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Ombi hilo limetolewa Februari 15, 2026 mkoani Pwani wakati wa mkutano mkuu uliowakutanisha wajane kutoka zaidi ya mikoa 18 nchini.

Katika mkutano huo, chama hicho kilipokea ufadhili wa mizinga 200 ya kufugia nyuki kutoka Lalji Foundation ya Dar es Salaam kwa lengo la kuwawezesha wajane kujishughulisha na ufugaji wa nyuki kama chanzo cha kipato.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bagamoyo, Zuena Ongele, alisema Serikali imepokea changamoto zinazowakabili wajane ikiwemo kunyimwa haki za mirathi, ukosefu wa mitaji ya kuendeleza biashara na kukosa ofisi kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa. Alisema zipo jitihada zinazoendelea kushughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mwenyekiti wa CCWWT, Rabia Moyo, alisema mkutano huo ulikuwa na lengo la kutathmini mafanikio na changamoto za chama pamoja na kutoa elimu katika masuala ya sheria, afya, saikolojia na uchumi ili kuwawezesha wajane kujitegemea. Aliongeza kuwa chama kitaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi nyingine kuboresha ustawi wa wajane nchini.

Mratibu wa Mradi kutoka Lalji Foundation, Judith Katano, alisema mizinga hiyo 200 itagawanywa katika mikoa mbalimbali ili kuwafikia wajane wengi zaidi na kuwasaidia kuzalisha asali pamoja na bidhaa nyingine zitokanazo na nyuki. Alisema mradi huo pia utaambatana na mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki ili kuhakikisha wanufaika wanapata tija inayotarajiwa.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo ya ufugaji nyuki, Vincent Mnaya kutoka Tanzania Forest Services Agency (TFS), aliwataka wananchi hususan vijana kuchangamkia fursa ya ufugaji wa nyuki akieleza kuwa ni biashara yenye kipato kizuri na inayoweza kufanyika kwa gharama nafuu ikiwa itasimamiwa vizuri.

Naye Katibu Mkuu wa CCWWT, Sabrina Tenganamba, alitoa wito kwa wanandoa kuthaminiana na kuishi kwa upendo wakiwa hai, akisema kukosekana kwa maandalizi mazuri ya maisha ya familia mara nyingi husababisha changamoto kwa wanawake wanapobaki wajane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *