Dar es Salaam. Droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu wa 2025/26 itafanyika kesho Jumanne, Februari 17, 2026, katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jijini Cairo, Misri.

Droo ya Kombe la Shirikisho itaanza saa 8:00 mchana huku droo ya Ligi ya Mabingwa ikifuata saa 9:00 alasiri. Mbali na kuamua nani atacheza na nani katika robo fainali, pia itaweka wazi njia ya timu kuelekea fainali ya mashindano yote mawili.

Timu zilizofuzu hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika msimu wa 2025/2026. Picha na Mtandao

Taswira ya Ligi ya Mabingwa

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, tayari timu zote nane zimehakikisha tiketi ya robo fainali. Katika kundi A, Pyramids FC ya Misri na RS Berkane ya Morocco ndizo zimetinga robo fainali.

Kundi B, mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly, wamefuzu, wakati AS FAR ya Morocco nayo ikifanikiwa kupenya na kuwatupa nje waliokuwa wapinzani wao wa karibu Yanga waliomaliza kwa pointi nane.

Katika kundi C, Klabu ya Al Hilal Omdurman ya Sudan na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zimetinga robo fainali baada ya timu zote kupata ushindi katika mechi zao za mwisho na kujihakikishia kutinga hatua hiyo.

Kundi D, Esperance de Tunis ya Tunisia imefuzu, pamoja na Stade Malien ya Mali huku ikishuhudiwa Simba ya Tanzania na Petro de Luanda ya Angola zikiaga mashindano.

Hadi sasa, timu zilizothibitisha kucheza robo fainali ni Pyramids FC, Al Ahly, Stade Malien, Al Hilal Omdurman, Mamelodi Sundowns, RS Berkane, AS FAR na Esperance de Tunis.

Mashabiki sasa wanasubiri kwa shauku droo ya Jumanne ambayo inaweza kuibua miamba kukutana mapema katika hatua ya mtoano.

Timu zilizofuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025/2026. Picha na Mtandao

Zilizofuzu robo fainali Kombe la Shirikisho

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, timu zilizofuzu robo fainali ni USM Alger ya Algeria, Olympic de Safi na Wydad Casablanca za Morocco, CR Belouizdad, AS Otoho ya Congo, Maniema ya DR Congo pamoja na Zamalek na Al Masry za Misri.

Misri na Morocco zinaongoza kwa idadi ya wawakilishi katika hatua hii, zikitoa wawakilishi wawili kila mmoja katika mashindano yote mawili ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *