Wakati mjadala wa maendeleo barani Afrika mara nyingi umejikita katika swali la upatikanaji wa fedha, wataalamu wa uchumi wa kilimo wanasema tatizo kubwa zaidi si kukosekana kwa mahitaji ya mitaji au mitambo bali ni kukosekana kwa upatikanaji wake.
“Afrika haina tatizo la uhitaji wa vifaa; ila tatizo letu ni namna ya kuvipata,” amewahi kueleza Profesa Andrew Temu, mchumi wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Katika mazingira hayo, Kampuni ya Equity for Tanzania Limited (EFTA) imezindua rasmi Hatifungani ya Kampuni (Corporate Bond) chini ya Mpango wa Hatifungani wa Muda wa Kati (Medium-Term Note Programme) wa jumla ya Shilingi bilioni 50, uliopitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na kuandaliwa kwa mujibu wa kanuni za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Mtaji wa muda mrefu kwa mashine za uzalishaji
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay, hatua hiyo inalenga kulinganisha mtaji wa muda mrefu na mali zinazozalisha mapato kwa muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Nicomed Bohay akizungumza wakati wa uzindunzi wa Hatifungani ya EFTA. Tukio hilo lilifanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam katika Hotel ya Kilimanjaro Hyatt Regency.
“Mashine tunazofadhili kama matrekta, magari ya biashara na mitambo ya viwandani huzalisha mapato kwa miaka kadhaa. Kuzifadhili kwa mikopo ya muda mfupi huweka shinikizo la ukwasi. Kupitia Hatifungani hii, tunaleta muundo wa mtaji unaolingana na miaka ya uzalishaji wa kiuchumi ya Mashine hizo,” amesema Bohay.
Takwimu zinaonyesha kuwa Afrika ina wastani wa takribani matrekta mawili kwa kila hekta 1,000 za ardhi inayolimika, ikilinganishwa na zaidi ya 100 katika baadhi ya nchi za Asia. Profesa Temu anaeleza kuwa pengo hilo si takwimu tu, bali linaashiria upotevu wa fursa za uzalishaji, hasara baada ya mavuno, kipato kidogo kwa wakulima na fursa ambazo hazijatumika kikamilifu.
Wafanyakazi wa EFTA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi rasmi wa Hatifungani ya EFTA ya Sh 50 bilioni jijini Dar es Salaam, wakionesha mshikamano na dhamira ya kuimarisha ufadhili wa muda mrefu kwa sekta za uzalishaji nchini
Katika nchi nyingi za Afrika, sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya nusu ya nguvu kazi, lakini hupokea chini ya asilimia tano ya mikopo rasmi ya benki. Hali hii, kwa mujibu wa wachambuzi, inaonyesha umuhimu wa mifumo mbadala ya ufadhili kama leasing (ukodishaji wa Mashine).
Ukopeshaji wa mashine kama suluhisho la kimuundo
Profesa Temu amekuwa akisisitiza kuwa mikopo ya mashine (leasing) hubadilisha swali kutoka “nani anaweza kumudu kununua?” kwenda “nani anaweza kutumia kwa tija?” Tofauti hiyo, kwa wataalamu wa maendeleo, ni ya msingi katika kuongeza tija hasa kwa wakulima wadogo na wajasiriamali wa vijijini.
EFTA inajikita katika ufadhili wa Mashine zinazozalisha mapato kupitia mfumo wa mikopo ya mashine (leasing). Kwa Bohay, mtaji utakaopatikana kupitia Hatifungani utaongeza uwezo wa kampuni kupanua wigo wa huduma hizo katika sekta za kilimo, usafirishaji, ujenzi, uchakataji wa mazao na nishati jadidifu.
“Lengo letu ni kuhakikisha mtaji tunaokusanya unaingia moja kwa moja kwenye uchumi halisi kwenye matrekta mashambani, mitambo kwenye viwanda na magari yanayosafirisha bidhaa,” amesema.
Riba shindani sokoni
Moja ya mambo yanayovutia wawekezaji katika Hatifungani ya EFTA ni kiwango cha riba kinachotolewa, ambacho kimeelezwa kuwa ni cha juu na chenye ushindani ikilinganishwa na baadhi ya fursa nyingine za uwekezaji wa mapato ya kudumu (fixed income) zinazopatikana kwa sasa sokoni.
Wajumbe wa jopo la majadiliano wakichangia mada wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya EFTA ya Sh 50 bilioni jijini Dar es Salaam, wakijadili umuhimu wa mtaji wa muda mrefu katika kuimarisha sekta za uzalishaji na kukuza masoko ya mitaji nchini.
Wachambuzi wa masoko ya mitaji wanaeleza kuwa katika kipindi ambacho baadhi ya hati za uwekezaji zinatoa mapato ya wastani, toleo la Hatifungani za EFTA limejitokeza kama chaguo lenye mvuto kwa wawekezaji wanaotafuta mapato bora ndani ya mfumo uliodhibitiwa kisheria.
Kwa mujibu wa Bohay, muundo wa riba umezingatia hali ya soko pamoja na uimara wa mali zinazofadhiliwa.
“Tumejenga toleo hili juu ya misingi ya usimamizi madhubuti wa hatari na mashine halisi zinazozalisha mapato. Tunaamini linatoa thamani kwa wawekezaji huku likiendelea kuwa endelevu,” amesema.
Changamoto za mtaji kwa taasisi za ukopeshaji wa mashine
Hata hivyo, Profesa Temu anaonya kuwa taasisi nyingi za ukopeshaji wa mashine barani Afrika bado zina mtaji mdogo, hali inayozilazimisha kutoa mikopo ya muda mfupi na kwa gharama kubwa.
Kilimo, kwa asili yake, kinahitaji mtaji wa uvumilivu (patient capital) unaoweza kuruhusu muda wa miaka mitano hadi saba kwa mitambo mikubwa, sambamba na mzunguko wa msimu wa kilimo.
Katika muktadha huo, mpango wa Hatifungani wa Sh bilioni 50 wa EFTA unaonekana kama hatua ya kujenga msingi imara wa mtaji wa muda mrefu kupitia soko la ndani la mitaji, badala ya kutegemea tu mikopo ya muda mfupi ya benki.
Kuimarisha soko la mitaji na uchumi
Utoaji wa Hatifungani chini ya mfumo rasmi wa MTN unalazimisha uwazi, utoaji wa taarifa za kifedha kwa wakati na uwajibikaji kwa wawekezaji, mambo ambayo wataalamu wanasema yanaimarisha taasisi pamoja na mfumo mzima wa kifedha.
Aidha, hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa ushiriki wa taasisi zisizo za benki katika soko la mitaji, jambo linalosaidia kupanua vyanzo vya mtaji na kupunguza utegemezi wa mikopo ya muda mfupi.
Kwa mtazamo mpana wa maendeleo, wataalamu wanaona ukopeshaji wa mashine za uzalishaji si tu kama bidhaa ya kifedha, bali kama nyenzo ya sera ya viwanda, ajira kwa vijana na hata kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi ya mashine zenye ufanisi zaidi.
Ikiwa mpango huu utafanikiwa, utaunganisha akiba za wawekezaji wa ndani na mahitaji halisi ya mashine za uzalishaji nchini, hatua ambayo inaweza kusaidia kupunguza pengo la tija lililopo katika sekta muhimu kama kilimo, ujenzi, usafirishaji, madini, biashara ndogo na za kati.
Swali linalobaki, kama anavyouliza Profesa Temu, si kwamba mahitaji hayapo — changamoto ni namna ya kupata majawabu ya mahitaji hayo. Je masoko ya mitaji yanayoanzishwa yatakuwa na uwezo wa kuyahudumia mahitaji hayo kwa ufanisi na kwa muda mrefu?
Ikiwa mpango huu utafanikiwa, utaunganisha akiba za wawekezaji wa ndani na mahitaji halisi ya mali za uzalishaji nchini, hatua ambayo inaweza kusaidia kupunguza pengo la tija lililopo katika sekta muhimu kama kilimo na biashara ndogo na za kati.
Zaidi ya mchango wake katika maendeleo ya uchumi, Hatifungani ya EFTA pia inafungua fursa ya faida kwa wawekezaji. Kwa kiwango cha riba kilichoelezwa kuwa ni cha juu na chenye ushindani ikilinganishwa na baadhi ya bidhaa nyingine za mapato ya kudumu sokoni, wawekezaji wanapata nafasi ya kunufaika na mapato ya uhakika ndani ya mfumo uliodhibitiwa na kusimamiwa kisheria.
Kwa maneno mengine, wawekezaji hawachangii tu ukuaji wa sekta za uzalishaji, bali pia wanapata faida ya moja kwa moja kupitia mapato ya riba yanayolipwa kwa mujibu wa masharti ya Hatifungani. Muundo wake wa uwazi, usimamizi wa kisheria na ulinganifu wa mtaji wa muda mrefu unalenga kutoa mchanganyiko wa mapato yenye mvuto na nidhamu ya kifedha.
Swali linalobaki, Je taasisi na masoko ya mitaji yatajengwa kwa uwezo wa kuyahudumia mahitaji ya soko kwa ufanisi na kwa muda mrefu?
Kwa uzinduzi wa Hatifungani ya EFTA, hatua moja kuelekea kujibu swali hilo imeanza kuchukuliwa huku ikiunganisha maendeleo ya uchumi na fursa ya uwekezaji yenye tija kwa Watanzania.