#HABARI: Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa taarifa ya ajali ya kusikitisha iliyotokea jana Februari 15, 2026, majira ya saa 11:30 jioni, ambayo imesababisha vifo vya watu watano katika Machimbo ya Mchanga ya Bolbit katika Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Korogwe.

Chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa ngema ya udongo ambayo iliwafukia watu watano wakati wakiwa katika shughuli za uchimbaji. Jitihada za uokoaji zilizoshirikisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na wananchi, zilifanikiwa kuitoa miili ya watu watano ambayo
imehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe Vijijini Makuyuni kwa taratibu zingine.

Waliopoteza maisha ni Shabani Mrisho @Mwantembo, (31), mkulima na mkazi wa Makuyuni, Yusuph Abdalah @Kibaya, mkulima na mkazi wa Makuyuni, Juma Hatibu @Msikiti, (49), mkulima na dereva, mkazi wa Makuyuni, Nurdini Amiri @ Daffa, (30), mkulima na mkazi wa Makuyuni na Zamiru Miraji @Daffa, (35), mkulima na mkazi wa Makuyuni.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini kuzingatia misingi ya usalama mahali pa kazi ili
kuepuka majanga yanayoweza kuzitumbukiza familia katika madhara kama haya.

Pia, viongozi wa vijiji na mitaa wanahimizwa kusimamia maeneo haya ya machimbo kwa ukaribu ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika katika mazingira rafiki na salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *